Simba yaiponza JKT Queens

Muktasari:

  • Mechi hiyo hiyo ilikuwa ipigwe Januari 8, mwaka huu lakini JKT haikwenda Chamazi, kwa madai inajua mechi inachezwa Meja Jenerali Isamuhyo, huku viongozi wa klabu hiyo wakisisitiza hawakuwa na taarifa ya kuhamishwa kwa uwanja, kitu ambacho kimekanushwa na Kamati ya Soka la Wanawake ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kupitia taarifa iliyotolewa jana baada ya kikao.

WATETEZI wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), JKT Queens yamewakuta baada ya kulimwa fainali ya Sh3 milioni pamoja kupokwa pointi tano kutokana na kitendo cha kushindwa kutokea kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuvaana na Simba katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Mechi hiyo hiyo ilikuwa ipigwe Januari 8, mwaka huu lakini JKT haikwenda Chamazi, kwa madai inajua mechi inachezwa Meja Jenerali Isamuhyo, huku viongozi wa klabu hiyo wakisisitiza hawakuwa na taarifa ya kuhamishwa kwa uwanja, kitu ambacho kimekanushwa na Kamati ya Soka la Wanawake ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kupitia taarifa iliyotolewa jana baada ya kikao.

Taarifa hiyo inasema JKT ilikuwa inajua mechi hiyo inapigwa Azam kwani walijulisha kikao cha kabla ya mechi kilichofanyika siku moja kabla ya tarehe ya mchezo, na kwa kuvunja kanuni ya 32.1-3 ya Ligi ya Wanawake, maafande hao wamepokwa pointi tano na kupoteza mchezo huo ambao Simba inafaidika kwa kupata pointi tatu na mabao matatu.

Mbali na kupokwa taarifa hiyo inasema imetoza fainali JKT faini ya Sh3 milioni na kumfungia pia Katibu Mkuu wa timu hiyo, Duncan Maliyabwana akifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya michezo.

Kutokana na maamuzi hayo, JKT iliyokuwa kileleni imeporomoka ilipokuwa na pointi 21 hadi nafasi ya pili ikisaliwa na pointi 16, wakati Simba inapanda juu na kukalia uongozi wa WPL ikifikisha pointi 22, kila moja ikiwa imecheza mechi nane.
Katika hatua nyingine, Alliance Girls imejikuta ikiporomoka hadi mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo ikiipokea Geita Gold Queens ambayo imeshinda rufaa dhidi ya wapinzani wao hao kumchezesha mchezaji asiye halali katika pambano lililochezwa Desemba 20 na wenyeji Alliance kushinda mabao 2-1.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Alliance imepoteza mechi hiyo na kulimwa pia faini ya Sh500,000, ilihali Geita ikipewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu na kuifanya ifikishe pointi nne, ikiwa ni moja zaidi ya ilizonazo wapinzani wao ambao awali walikuwa na pointi sita kila ikicheza mechi nane hadi sasa.

Aidha mchezaji Nelly Kache aliyeiponza Alliance akilimwa fainai ya Sh500,000 kama aliyopigwa Meneja wa timu hiyo, Thereza Chacha anayedaiwa kutoa nyaraka zisizo halali za mchezaji huyo.

Ofisa Habari wa JKT, Masau Bwire alisema wameona taarifa hiyo ya TFF, lakini ni mapema mno kusema lolote hadi pale viongozi wa juu watakapokutana kujadili na kutoa tamko lao.

"Viongozi wa juu wa JKT watakutana na kujadili hukumu hiyo, kwani ndio kwanza tumepokea barua," alisema Masau.