Simba yacheza akili ndefu

HII ni akili ndefu. Unaambiwa uwepo wa makocha watatu Simba ambao ni Didier Gomes, Thierry Hitimana na Seleman Matola ni kete ya turufu itakayoinufaisha klabu hiyo iliyofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili katika misimu mitatu iliyopita.

Simba imemuongeza Hitimana katika benchi la ufundi awe msaidizi wa Gomes, lakini pia akatumike kama kocha mkuu katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, sababu kocha mkuu Gomes hana vigezo kwa sasa vya kuiongoza katika mechi zinazosimamiwa na Caf.

Aliyekuwa kocha wa Mtibwa Sugar, Mohamed Badru anaamini kila jambo hutokea kwa sababu na hilo litainufaisha sana Simba.

“Benchi la ufundi linapokuwa na makocha wenye ujuzi tofauti inasaidia kuwa na timu bora, wenzetu Ulaya ni jambo la kawaida ndio maana soka lao lina mvuto. Matola akikaa na Gomes na Hitimana vizuri wakiamua kutanguliza maslahi ya Simba watafanya maajabu makubwa sana,” alisema Badru.

“Ni vyema Simba walifanye hili kwa mwendelezo na lisiwe kwa dharura tu. Wakifaulu litawafunza wengine zaidi, naamini uongozi wao upo makini na unaweza ukabadilisha taswira ya soka kuwa la kisasa zaidi.”

Alisema Ulaya kuna makocha wa kikosi cha kwanza na cha pili na wakati wa mechi benchi linakuwa na walimu wengi, kila mmoja anapewa kazi kumsaidia mkuu wao ambaye anakuwa na uamuzi wa mwisho.

“Ili kocha mkuu afanikiwe ni lazima nyuma yake awe na wasaidizi wengi na ndio kitu ninachokiona kwa Simba, kwa sababu mpira wa kisasa timu siyo wachezaji tu, inatakiwa iwe na muunganiko wa idara zote,” alisema.

Naye beki wa zamani wa timu hiyo, Martin William alisema: “Wasiishie kuimarisha makocha tu, wamuajiri na mtu wa saikolojia wa timu ambaye atawajenga makocha hao watangulize maslahi ya klabu na namna ambavyo wachezaji wanapaswa kuishi kama mastaa pia kujieleza kwenye vyombo vya habari.”

Staa mwingine wa zamani wa timu hiyo, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema: “Nategemea kombinesheni ya makocha itakuwa na matunda uwanjani, kiukweli viongozi naona wameona mbali kutaka kuonyesha soka la kisasa zaidi kwa matendo.”


KIBURI CHA GOMES

Mzuka uliopo kambini kwa nyota wapya na wa zamani umemfanya Gomes kujiamini kuelekea msimu ujao. Nyota wapya Sadio Kanoute, Pape Sakho, Peter Banda, Kibu Denis, Yusuph Mhilu, Simson Mwanuke na Duncan pamoja na mastaa wa zamani kina Chris Mugalu, John Bocco, Ibrahim Ajibu, Thadeo Lwanga na mabeki Joash Onyango, Mohammed Hussein, Shomary Kapombe, Pascal Wawa na kipa Aishi Manula wanamfanya Gomes kuamini bado ana timu ya ubingwa licha ya kuwapoteza viungo Clatous Chama na Luis Miquissone waliouzwa Uarabuni.

“Wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri, kila mmoja anacheza vizuri kuipambania timu.. nadhani msimu ujao tutakuwa bora zaidi,” alisema Gomes.


Imeandikwa na Olipa Assa, Clezencia Tryphone na Ramadhan Elias