Simba yaanza kufumua timu, kushusha straika Seria A ya Italia

WAKATI mashabiki wa Simba wakiendelea kusononeka kutokana na chama lao kuwa na msimu mbaya safari hii, tofauti na misimu minne mfululizo iliyopita, lakini mabosi wao wamepanga kuwafanyia sapraizi ya kishindo kwa maandalizi ya msimu ujao.

Simba imepoteza mechi ya nusu fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Yanga na kupoteza tumaini la kutetea taji hilo iliyokuwa ikilishikilia kwa misimu miwili mfululizo, huku kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara zikiwapa nafasi kubwa watani wao.

Hata hivyo, mabosi wa klabu hiyo kupitia bilionea wao, Mohamed ‘Mo’ Dewji, wameanza kukuna vichwa mapema kwa ajili ya msimu ujao kwa kutaka kutembeza panga la maana katika kikosi chao likiwamo benchi la ufundi, lakini likianza kuzungumza na mastaa mbalimbali kuwaleta.

MO aliandika kwenye akaunti ya twita kuwa Simba imekuwa na msimu mbaya, hivyo wanahitaji mikakati ya kuijenga vizuri timu hiyo kwa msimu ujao kwa kurejesha heshima.

Achana na Victorien Adebayor wa USGN ya Niger ama Stephane Aziz Ki wa Asec Mimosas, huku ikiwa na uhakika wa kumleta, Moses Phiri kutoka Zambia, mabosi wa Simba wapo kwenye mipango ya kumshusha straika kutoka Nigeria anayepigia klabu ya Udinese ya Italia.

Ndio. Habari kutoka ndani ya Simba zinasema, mabosi wa klabu hiyo wameanza mazungumzo na straika huyo wa klabu hiyo ya Seria A, Isaac Succes Ajayi.

Kama dili hilo litafanikiwa itakuwa kama ni jibu la Simba dhidi ya watani wao, Yanga ambao msimu uliopita ilimleta, Saido Ntibazonkiza aliyewahi kucheza soka la kulipwa soka klabu ya NEC ya Uholanzi na kukipiga klabu kadhaa za Uturuki, Ufaransa na Poland.

Uongozi unasaka straika wa kuja kutatua tatizo la timu hiyo katika ufungaji mabao baada ya mastaa wake, Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu walioibeba msimu uliopita kupatwa na upepo mbaya na kuifanya timu kupoteza makali yake eneo la mbele.

Katika msimu uliopita wa Ligi ya Seria A, Isaac mwenye miaka 25 alicheza mechi 22 na kufunga mabao mawili, huku akiasisti mara saba, hii ikitokana na rekodi yake ya kuwa majeruhi kila mara tangu msimu uliopita.

“Kuna mazungumzo yanaendelea baina ya wakala wa mchezaji huyo (Isaac Success), ili kuona kama anaweza kuja Msimbazi, pia kuna mastaa wengine wanafuatiliwa, kwa lengo la kutaka kujenga kikosi bora kwa msimu ujao,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba.

Isaac amewahi kukipiga pia Watford iliyoshuka daraja msimu huu kutoka Ligi Kuu ya England hadi Championship, pia ameichezea Granada na Malaga za Hispania.

Licha ya chanzo hicho kusisitiza, Simba ya msimu ujao inasukwa kivingine kabisa ili kurejesha heshima nchini na kimataifa, bado kuna sintofahamu juu ya masilahi ya kumshawishi Mnigeria huyo kuja Tanzania.

Issac aliwahi kunukuliwa na gazeti la The Guardian la Uingereza Nov 26, 2016 akisema;”Mpira wa miguu unaweza kumfikisha mtu mahali popote katika maisha yake’, kuonyesha yeye ni kambi popote.

Inaelezwa Simba imeanza kufanya mipango ya kukifumua kikosi baada ya msimu huu kupoteza mataji yote mawili ya Ligi Kuu na Kombe la ASFC mbele ya Yanga, huku ikishindwa iking’olewa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kukwamisha robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, tofauti na mipango iliyokuwa nao awali.