Simba yaandaa sapraizi Kwa Mkapa

Muktasari:

  • Kapombe amesema wamepata muda mzuri wa kujiandaa na wana imani wanakwenda kufanya vizuri.

SIMBA imewaandalia sapraizi mashabiki wa timu hiyo, katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri utakaopigwa kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 3:00 usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, beki wa Simba, Shomari Kapombe amesema mchezo wa kesho ni sapraizi kwa mashabiki na wajitokeze kwa wingi ili kuhakikisha wanawasapoti na kupata ushindi katika mchezo wao wa nyumbani.

Kapombe amesema wamepata muda mzuri wa kujiandaa na wana imani wanakwenda kufanya vizuri.

"Ni robo fainali yetu ya tano malengo yetu ni kwenda nusu fainali msimu huu hivyo tunapambana kuhakikisha tunashinda na kuvuka hatua inayofuata japo haitakuwa michezo rahisi," amesema Kapombe.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alisema Simba inahitaji mabao mengi kwenye uwanja wa nyumbani na haitakata tamaa huku pia benchi la ufundi likifanya kila liwezekanalo kufanikisha mechi hiyo.

Ameongeza kuwa kuwakosa kambini Zanzibar baadhi ya nyota waliokuwa katika timu zao za Taifa kwa ajili ya mechi za kirafiki za FIFA Series, hakutaathiri chochote ingawa alitamani wawepo na kushiriki kwa pamoja.

"Mechi ya kesho ni kubwa kwa klabu zote mbili na nategemea mambo mazuri na sisi kama Simba tunajua tunacheza na timu kubwa hivyo tumechukua tahadhari zote, matokeo ya kesho yataamuliwa kesho," amesema Benchikha.

Kwa upande wa kocha wa Ahly, Marcel Koller amesema wachezaji majeruhi watakuwa pengo kwao japo haitaathiri chochote kwa kuwa wana kikosi kipana.

"Wachezaji wetu waliopata majeraha wana umuhimu mkubwa, lakini kutokana na upana wa kikosi chetu naamini kila mchezaji anajiamini na waliopo watafanya vizuri kwenye mechi ya kesho," amesema Koller.