Simba wawateka tena Maafande, wainyoosha tena

Muktasari:

Tangu Polisi Tanzania upande Ligi Kuu haujawahi kupata hata sare ikiwa ni kuchezea vipigo na leo tena imeangukia pua kwa bao 1-0.

Mwanza. Pamoja na soka safi na la ushindani waliloonesha Polisi Tanzania lakini imekubali tena kuwa 'mteja' kwa Wekundu wa Msimbazi, Simba baada ya kulala bao 1-0 leo.

Huu ni mchezo wa nne kwa timu hizo kukutana uwanjani kwenye mechi ya Ligi Kuu, ambapo Simba imeendelea kuwanyanyasa Maafande hao kwa vipigo tangu walipopanda daraja misimu misimu miwili.

Katika mchezo wa leo ambao umepigwa uwanja wa CCM Kirumba, kipindi cha kwanza ilishuhudiwa Simba wakitawala mechi hiyo na kufanikiwa kupata bao lililofungwa na Luis Miquisone dakika 27 kwa mpira wa faulo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mabadiliko ambapo Simba iliwatoa Mugalu, Bwalya na Yassin na kuingia Kagere, Nyoni na Hassan Dilunga ambao hawakubadili chochote katika matokeo ya awali.

Polisi Tanzania wao walimtoa Daluwesh Saliboko na nafasi yake kuchukuliwa na Jimmy Shoji mabadiliko ambayo pia hayakuwa na faida zaidi ikiwamk kusawazisha au kupata ushindi.

Hata hivyo kabla ya dakika 90 za Mwamuzi, Ahamad Simba kutoka Kagera kumalizika, Polisi Tanzania walipata nafasi moja ambayo ilikuwa pengine iwape bao, lakini walijikuta wakikumbana ngome imara ya Wekundu walioondosha hatari hiyo ikiwa ni dakika ya 72.

Pia Simba nao watajilaumu kwa nafasi waliyopata ambapo Kagere akiwa eneo safi la kufunga bao, alishindwa kumalizia vyema pasi ya John Bocco baada ya mpira wake kupaa juu ikiwa ni dakika ya 75.

Kwa matokeo hayo Simba wanaendelea kujikita keleleni kwa pointi 70, huku Maafande wakibaki na alama zao 41 katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu unaoelekea ukingoni.