Simba wavunja ukimya kutimuliwa Gomes

Muktasari:
- Simba ambayo ilipata ushindi ugenini, iliruhusu kipigo nyumbani na kuondoshwa kwenye Ligi ya mabingwa ambapo sasa imeangukia kwenye kombe la Shirikisho.
Uongozi wa klabu ya Simba umevunja ukimya juu ya kutimuliwa kwa kocha wake mkuu, Didier Gomes.
Tangu Jumapili baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-1 nyumbani na kuondoshwa kwenye Ligi ya mabingwa, kumekuwa na sintofahamu juu ya kibarua cha kocha Gomes na benchi la ufundi la timu hiyo.
Katika mahojiano na Mwananchi Digital, Rais wa Simba, Murtaza Mangungu amesema bado klabu haijatoa tamko kuhusu hilo.
"Tuko kwenye hatua kikao, kujadiliana kuhusu hilo na kufanya tathimini ya mechi yetu iliyopita.
"Pia tunakusanya taarifa na kusikiliza maoni ya wadau wetu, tukikamilisha tutatoa tamko," amesema Mangungu.
Ingawa habari za ndani zinasema Gomes wakati wowote kuanzia sasa anaweza kutupiwa virago, jambo ambalo Mangungu amesema watalitolea tamko muda muafaka ukifika.
Kuhusu tathimini ya mechi yao ya Jumapili, Mangungu amesema ni bahati mbaya na sasa focus yao ni kwenye mashindano yajayo ya kombe la Shirikisho.
"Tunasubiri ratiba itoke tujue tunaanzia wapi," amesema.
Baada ya mechi hiyo baadhi ya watu wenye ushawishi ndani ya klabu hiyo akiwamo Mohammed 'Mo' Dewji na Magori kupitia mitandao ya kijamii wali-twiti kuhusu mchezo huo huku baadhi wakiandika kana kwamba kuna dalili za hujuma, Mangungu amesema hao ni wanachama wa Simba na wana haki ya kutoa maoni yao.
"Uongozo wa Simba ni bodi ambayo ina wajumbe na menejimenti inayosimamiwa na bodi, wengine ni wana simba ambao wana haki ya kutoa maoni na ni haki yao kikatiba,".
Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Mirambo anasema kocha anaajiliwa na kutimuliwa hivyo suala la kuondolewa kwa Gomes ni kawaida japo uongozi umechukua uamuzi kwa kuchelewa.
“Kama kweli katimliwa au wanampango wa kufanyahivyo wamechelewa kwasababu kabla ya mashindano walikuwa na taarifa juu ya CV anazotakiwa kuwanayo na kuamua kutafuta mtu mwingine walipaswa kumuacha na kumpa majukumu huyo aliyena vigezo,” anasema.
Naye kocha wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kiwelu anasema ilikuwa wazi kwamba lawama zote zinakwenda kwa kocha japo wachezaji pia wamefanya makosa ila ndio maisha ya makocha.