Simba wapaa Kigoma, Gomes awataja Barbara, Mo Dewji

Kikosi cha Simba, kitaondoka saa 9:45 alasiri na shirika la ndege la Air Tanzania kuelekea Kigoma katika mechi ya fainali ambayo itachezwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika Julai 25.

Msafara wa Simba ulifika katika uwanja wa ndege saa 7:40 mchana wakitokea kambini kwao huku wakionekana kuwa na morali kubwa ya mchezo huo.

Simba katika kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi hiyo ya fainali dhidi ya Yanga, asubuhi ya leo walifanya mazoezi katika Uwanja wao wa Mo Simba Arena uliopo Bunju.

Kabla ya kuanza safari kocha wa Simba Didier Gomes alionekana kuwa na matumaini makubwa ya kurudi na ushindi katika mechi hiyo akieleza sababu kubwa ya maandalizi mazuri ambayo wameyafanya

Gomes alisema ni muhimu kwa timu yake kushinda mataji yote ya ndani kwani wameshinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara nne mfululizo na wanataka kufanya hivyo katika kombe la Shirikisho (ASFC),  kwa kuchukua mara mbili mfululizo.

Gomes alisema mara zote huwa anazungumza anatamani kuona mashabiki wa Simba muda wote wanakuwa na furaha kwani hilo ni jambo muhimu kwao.

Alisema wanaenda kucheza mechi hiyo ya fainali kwa mambo matatu, jambo la kwanza ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohamed Dewji pili Ofisa Mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez ambaye muda wote wapo nae katika kuwapa nguvu.

"Jambo la tatu ni mashabiki kwani ni muhimu Simba kuchukua mataji na sawa hakuna kitu uwepo wa timu hii bila ya wimbi la mashabiki wake na wanatakiwa kwenda kuwapa nguvu katika mechi ya fainali," anasema Gomes na kuongeza;

"Jumatatu asubuhi mashabiki wa Simba wanatakiwa kujitokeza na kuwapa nguvu kwani wanaamini katika malengo yao watarudi na kombe kwani wamefanya maandalizi ya kutosha ya mchezo huo."

Simba wanaingia katika mechi hiyo akiwa na kumbuka ya kufungwa mechi ya mwisho ya ligi waliokutana na Yanga wakifungwa bao 1-0, lililofungwa na Zawadi Mauya.

Rekodi nzuri kwa Simba kwenye mchezo huu walipokutana na Yanga mara ya mwisho kwenye kombe la Shirikisho (ASFC), waliwafunga Yanga mabao 4-1.