Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba waikalia kooni Dabi, waitumia ujumbe Bodi ya Ligi

Muktasari:

  • Kupitia taarifa hiyo, Simba imewakumbusha mashabiki kutunza tiketi zao walizonunua kwaajili ya mchezo wa Machi 8, 2025 ambazo hazikutumika baada ya mchezo huo kuahirishwa na kuwataka mashabiki wengine ambao hawakununua tiketi kununua mara tu Bodi ya Ligi itakapotangaza kuanza kwa zoezi hilo.

LICHA ya kuwa Yanga SC ambayo ni timu mwenyeji wa mchezo wa Dabi ya Kariakoo uliopangwa kuchezwa Juni 15, 2025 kusema hadharani haitacheza hadi matakwa yao manne yatakapofanyiwa kazi, imekuwa tofauti kwa wapinzani wao Simba ambao mapema leo Juni 10, 2025 imetoa taarifa kwa umma ikiwakumbusha mashabiki kuhusu mchezo huo na pia kutuma ujumbe kwa Bodi ya Ligi.

Kupitia taarifa hiyo, Simba imewakumbusha mashabiki kutunza tiketi zao walizonunua kwaajili ya mchezo wa Machi 8, 2025 ambazo hazikutumika baada ya mchezo huo kuahirishwa na kuwataka mashabiki wengine ambao hawakununua tiketi kununua mara tu Bodi ya Ligi itakapotangaza kuanza kwa zoezi hilo.

“Klabu ya Simba inatoa taarifa kwa Wanachama, Wapenzi, na Umma kuwa mchezo nambari 184 dhidi ya Yanga uliopangwa kufanyika tarehe 15/6/2025 upo kama ulivyopangwa.

“Tunawasihi msihadaike na kelele za mitaani, wale ambao walinunua tiketi za mechi ya tarehe 8/3/2025 wazitunze kwa ajili ya matumizi ya mchezo huo na wale ambao hawajanunua tiketi wajiandae kununua baada ya tangazo la Bodi ya Ligi. Twendeni tukaujaze Uwanja wa Mkapa,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeikumbusha Bodi ya Ligi kufuata taratibu za uendeshaji wa Ligi hiyo na kutoa ripoti ya uchunguzi hadharani na wote waliohusika na vurugu zilizofanyika usiku wa machi 7, 2025 kuamkia siku ya Dabi kuchukuliwa hatua.

“Inafahamika wazi kuwa Ligi Kuu ya NBC inajumuisha timu 16 na si ligi ya timu moja, kwa mujibu wa taratibu kabla ya kuanza msimu, vilabu vyote 16 hushiriki vikao na kutoa mapendekezo ya kuboresha kanuni na taratibu ili kuimarisha ligi yetu, hivyo wenye hoja wafuate taratibu husika.

“Tunaomba Bodi ya Ligi na TFF watoe hadharani ripoti ya uchunguzi juu ya wale wote waliohusika kuharibu mechi ya ligi jioni ya tarehe 7/3/2025 na wachukuliwe hatua stahiki na mamlaka husika.

“Kutotolewa kwa ripoti na kutochukuliwa hatua kwa wanaoendelea kuchochea ghasia ni sawa na kulinda uharamia katika mpira ambao unatia dosari mafanikio yaliyopo katika tasnia ya mpira wa miguu nchini kwa sasa,” imefafanua taarifa hiyo.