Simba vs JKT usiguse rimoti

LEO Jumanne kuanzia saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex utashuhudiwa mtanange wa Fainali ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake kati ya JKT Queens na Simba Queens ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Michuano hiyo mipya iliyoanza msimu huu inashirikisha timu nne za juu ambazo ni mabingwa wa Ligi Kuu JKT Queens, Simba Queens, Fountain Gate Princess na Yanga Princess.
JKT ndio ilikuwa timu ya kwanza kutinga fainali baada ya kuichapa Fountain mabao 5-0 huku Simba ikiitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu.
Timu hizo zilipokutana msimu uliopita kwenye Ligi, duru ya kwanza JKT iliondoka na ushindi wa pointi tatu mbele ya Simba na ziliporudiana zilitoka sare ya bao 1-1.
Kiungo mkabaji wa JKT, Donisia Minja na mshambuliaji Stumai Abdallah ni miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa kwenye mchezo huo kwani ni hatari zaidi wanapokuwa langoni.
Kwa Simba kulingana na kikosi kilichocheza nusu fainali dhidi ya Yanga kuna wachezaji kama Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ ambaye ni mkongwe kwenye kikosi hicho, Vivian Corazone na Elizabeth Wambui ambao ni hatari kwenye kupeleka mashambulizi.
Kocha msaidizi wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema kikosi kipo tayari kwa mechi ya leo na makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita wameyarekebisha; “Tunafahamu ni mchezo mgumu kwetu kwa sababu tunacheza na timu nzuri, tunaamini tutapata ushindi na makosa yote yaliyotokea kwenye mchezo uliopita tumefanyia kazi.”
Kwa upande wa Kocha wa JKT, Esther Chabruma alisema haitakuwa mchezo rahisi kwao lakini watapambana kuhakikisha wanashinda na kubeba taji hilo huku wakitoa burudani kwa mashabiki.
“Kwanza nawapongeza Shirikisho la Soka (TFF) kwa kuleta mashindano haya kama wanaume, pili naamini kikosi changu kitafanya vizuri mchezo wa fainali,” alisema Chabruma ambaye amebeba ubingwa wa CECAFA.
Fainali hiyo itachezeshwa na mwamuzi wa kati, Tatu Mwalogo kutoka Tanga akisaidiana na Glory Tesha na Zawadi Yusuph kutoka (Dar es Salaam) huku mechi ya mshindi wa tatu kati ya Yanga na Fountaun Gate, ni Jonesia Rukyaa (Kagera) akisimama kati, akisaidiana na Wema Kalinga na Fatuma Mambo.