Simba Utamu, Bocco Mtamu

Muktasari:
- Simba imefikisha pointi 38, tano zaidi na ilizonazo Azam iliyoifunga Ndanda mabao 3-1 juzi Jumamosi usiku na pointi saba mbele ya watani zao wa jadi, Yanga yenye alama 31.
SIMBA mziki mnene. Chama hilo limezidi kung’ara katika mbio zake za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya jana Jumapili kuishindilia Ruvu Shooting mabao 3-0 huku straika aliye pia nahodha wake, John Bocco ‘Adebyor’ akizidi kunoga.
Bocco alifunga mara mbili na kumfanya afikishe mabao tisa mpaka sasa katika ligi hiyo nyuma ya Emmanuel Okwi anayongoza kwa mabao 12 ambaye jana alishindwa kumaliza mchezo baada ya kuumizwa na beki wa Ruvu, Mau Bofu.
Bao jingine katika mchezo huo liliwekwa kimiani na kiungo Mzamiru Yassin na kuifanya Simba izidi kupanua pengo la pointi dhidi ya timu zinazoifukuza kileleni.
Simba imefikisha pointi 38, tano zaidi na ilizonazo Azam iliyoifunga Ndanda mabao 3-1 juzi Jumamosi usiku na pointi saba mbele ya watani zao wa jadi, Yanga yenye alama 31.
Katika mchezo huo wa jana uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Ruvu iliyofungwa mabao 7-0 kwenye mchezo wa duru la kwanza dhidi ya Simba, ilijikuta ikipoteza wachezaji wake wawili kizembe kwa kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi, Hans Mapema.
Mau Bofu alionyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumpiga kooni Okwi na kumfanya kinara huyo wa mabao wa VPL kuzimia na kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo katika dakika ya 23.
Bofu alishaonyeshwa kadi ya njano mapema kabla ya tukio hilo lililowastajabisha mashabiki waliofurika uwanjani hapo na kutoa faida kwa Simba iliyokuwa imepata bao la kuongoza dakika ya 22 kupitia Bocco aliyeunganisha kona ya Shiza Kichuya.
Mchezaji mwingine aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu ni Adam Ibrahim dakika za lala salama kwa kumchezea vibaya Shiza Kichuya.
Kwa kifupi Ruvu waliingia uwanjani wakiwa wamekamia pambano hilo pengine kutaka kufuta aibu ya kufungwa mabao 7-0 katika mechi ya kwanza na kuishia kucheza rafu za mara kwa mara kwa wachezaji wa Simba.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kila timu ikishambulia kusaka bao la mapema, lakini ni Simba waliowazidi ujanja wapinzani wao na kujipatia bao la kuongoza ambalo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Ruvu kushindwa kumuzia Bocco asifunge.
Bocco alifungwa kwa kichwa, huku akiwa amekumbatiwa na beki wa Ruvu na kurudi tena kambani katika kipindi cha pili dakika ya 75 baada ya awali Mzamiru kufunga bao tangu dakika ya 66 akiunganisha pasi murua ya Kichuya aliyeng’ara jana.
Katika mechi ya jana Simba ilitumia mfumo wa 4-4-2 na kuwafunika wapinzani wao na hasa baada ya mabadiliko ya mapema kipindi cha pili yaliyofanywa na Kocha Pierre Lechantre la kumtoa Said Ndemla na kumwingiza Mwinyi Kazimoto.
Ruvu nao katika kipindi hicho ilimtoa Issa Kanduru na kumwingiza Yusuph Mguya pia kumtoa Full Maganga Mussa kumpisha Jamal Masoud kabla ya Simba kumtoa Bocco ili kumpisha Nicholas Gyan.
Ruvu wanaweza kujilaumu kwa kukosa mabao ya wazi dakika za lala salama kwa Abdulrahman Mussa na Masoud kupoteza nafasi za wazi.
Ushindi wa jana ni wa tano mfululizo kwa Simba tangu Kocha Joseph Omog atimuliwe, ikiwa imefunga jumla ya mabao 19 bila kuruhusu wavu wao kuguswa katika mechi hizo. Simba ilianza kwa kuifunga Ndanda mabao 2-0, kisha ikaichapa Singida United mabao 4-0 na kuizima Kagera Sugar 2-0 kabla ya wiki iliyopita kuilaza Mwadui mabao 2-0 na jana kupata ushindi huo wa 3-0.
Tamu tamu hoi
Katika mechi nyingine, Mbao FC iliilaza Kagera Sugar mabao 2-1 huku Mtibwa ikilala Shinyanga mabao 2-1 kwa Stand United.
Wafungaji wa Mbao walikuwa James Msuva na Habib Kiyombo huku Atupele Green akiifungia Kagera.
Mtibwa ilifunga kupitia Seleman Kihimbwa kabla ya Birigimana Babikaule na Tariq Seif kuizamisha.