Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hoja sita kuamua Dabi ya Kariakoo

HOJA Pict

Muktasari:

  • Katika kikao hicho ambacho kimepangwa kufanyika Jumatatu hii kwenye Ofisi za TPLB zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam, kuna hoja sita nzito mezani za kujadiliwa ambazo zitaonyesha mwanga endapo mchezo huo utachezwa Juni 15 mwaka huu kama ulivyopangwa au nini kitatokea.

WAKATI sintofahamu ikiendelea kutanda juu ya hatma ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo, viongozi wa Yanga wameitwa makao makuu ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).

Katika kikao hicho ambacho kimepangwa kufanyika Jumatatu hii kwenye Ofisi za TPLB zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam, kuna hoja sita nzito mezani za kujadiliwa ambazo zitaonyesha mwanga endapo mchezo huo utachezwa Juni 15 mwaka huu kama ulivyopangwa au nini kitatokea.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaeleza TPLB imewaita viongozi hao mezani, kuzungumza nao kwani Yanga ndiyo timu mwenyeji wa mchezo huo.

Kwenye kikao hicho, Bodi ya Ligi inawataka viongozi hao wa Yanga kueleza hatua ya maandalizi ya mchezo huo ambao umepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 11:00 jioni.

“Kutakuwa na kikao cha Bodi na timu mwenyeji kitakachofanyika Jumatatu Juni 9, 2025 na kuanzia hapo tutajua nini kitaendelea. Hiki ni kikao cha kawaida tu cha maandalizi ya mchezo,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya TFF.

Kikao hicho kitafanyika wakati Yanga bado ikiwa kwenye msimamo mkali wa kutocheza mchezo huo, kwa madai chombo hicho hakijayafanyia kazi masuala yaliyosababisha kuahirishwa kwa ule wa kwanza uliopangwa kufanyika Machi 8, 2025.

Hata hivyo, Yanga inaona kikao hicho ni kama mtego, kwani hakujawahi kufanyika mkutano wa namna hiyo utakaoukutanisha uongozi mzima wa juu wa Yanga.

Kwenye kikao hicho Yanga imetakiwa kuwakilishwa na kamati nzima ya utendaji kuanzia Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, Makamu wake, Arafat Haji na wajumbe wa kamati ya utendaji.

Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara toleo la 2024, kanuni ya 17 inayozungumzia Taratibu za Mchezo, kifungu cha 48 chenye vifungu vingine vidogo, kuna hoja sita zinahusu kikao hicho.

Kanuni hiyo inaanza kwa kueleza hivi; “(48) Mchezo wowote wa Ligi Kuu lazima uandaliwe kwa ukamilifu wa huduma muhimu za msingi za mchezo kuchezwa kama usalama, huduma ya kwanza, daktari, gari la wagonjwa, waokota mipira na uwanja (pitch) uliotayarishwa kwa kufuata sheria za uwanja wa kuchezea.”

Kanuni hiyo imeendelea kufafanua kupitia vifungu vidogo kwamba: “48.1 Klabu ya Ligi Kuu inawajibika kwa shughuli zote za maandalizi ya mchezo ikiwemo uuzaji wa tiketi za kuingilia uwanjani kwa njia ya elektroniki.

“48.2 Muongozo wa uuzaji tiketi utatolewa na TFF/TPLB ambapo klabu itawajibika kutafuta mzabuni wake na kuwasilisha taarifa zake kwa TFF/TPLB.

“48.3 Maandalizi na ugawaji wa vitambulisho vya msimu, mialiko ya watu maalum (VVIP) na mpangilio wa jukwaa la watu maalum, yatakuwa chini ya mamlaka ya TFF/TPLB.

“48.4 Klabu ya Ligi Kuu inawajibika kuutangaza kila mchezo wake wa Ligi kwa njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari.

“48.5 Klabu mwenyeji inapaswa kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa sauti uwanjani kwa ajili ya kutoa matangazo muhimu na burudani kwa watazamaji.”

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara duru la pili, bado umeacha maswali iwapo utakuwepo au la, huku baadhi ya nyota wa Simba na Yanga walioitwa timu ya Taifa Stars wakirejea kutoka Afrika Kusini kujiunga na wenzao baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Wasauzi uliopigwa nchini humo kumalizika kwa suluhu, Ijumaa iliyopita.

Kikosi cha Yanga kimekuwa kikiendelea na mazoezi na inaelezwa ni kujiandaa na michezo mitatu iliyosaliwa nayo, miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons (Juni 18) na Dodoma Jiji (Juni 22), pamoja na ule wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Singida Black Stars (Juni 28).

Yanga ambayo ndiyo timu mwenyeji wa mchezo huo wa Dabi ya Kariakoo, imekuwa kimya kwa muda mrefu kuuzungumzia huku msisitizo wake ni kwamba haichezi.