Simba tishio jamani, yafunika Afrika

Muktasari:

USHINDI wa mabao 2-0 iliopata ugenini dhidi ya Jwanenga Galaxy juzi Jumapili katika mechi za mwanzo za hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, umeshtua wakubwa ambao walidhani kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Jose ndiyo mwisho.

USHINDI wa mabao 2-0 iliopata ugenini dhidi ya Jwanenga Galaxy juzi Jumapili katika mechi za mwanzo za hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, umeshtua wakubwa ambao walidhani kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Jose ndiyo mwisho.

Ushindi wa Simba umezifunika timu 10 vigogo vya soka barani Afrika. Timu hizo 10 licha ya uzoefu, uwekezaji mkubwa na ubora wa vikosi vyao zimeshindwa kufua dafu katika mechi hizo zilizochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo kutokuwa na matumaini makubwa kama zitatinga katika hatua ya makundi au la.

Kati ya timu 13 ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kutinga katika hatua ya makundi, ni tatu zilizoweza kupata matokeo mazuri ambayo yanaziweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata kwani zimepata ushindi wa ugenini. Klabu tatu ambazo angalau zimeonyesha jeuri kama ya Simba ni Raja Casablanca ya Morocco na Zamalek ya Misri

Wakati Simba ikiichapa Jwaneng Galaxy ugenini kwa mabao 2-0, Raja Casablanca ilipata ushindi kama huo dhidi ya LPRC Oilers ya Liberia ikiwa ugenini, wakati Zamalek iliyokuwa Kenya kucheza na wenyeji wao Tusker, ilipata ushindi wa bao 1-0 tena kwa taabu.

Vigogo 10 ambao hali zao ni tete ni mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri, Etoile Du Sahel na Esperance za Tunisia, CR Belouizdad na ES Setif (Algeria), Wydad Casablanca (Morocco), TP Mazembe (DR Congo), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Al Hilal (Sudan) na Petro Atletico (Angola)

Al Ahly ililazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini na US Gendarmerie ya Niger wakati Etoile Du Sahel ilipata sare kama hiyo nchini Rwanda na wenyeji wao APR huku CR Beloizdad ikichapwa mabao 3-1 ugenini na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

TP Mazembe ilibanwa ugenini huko Afrika Kusini kwa kutoka sare ya bila kufungana na Amazulu, Mamelodi Sundowns ikatoka sare ya mabao 2-2 nchini DR Congo na AS Maniema na ES Setif ilichabangwa mabao 3-1 ugenini huko Mauritania na timu ya Nouadhibou.

Hearts of Oak ya Ghana iliyokuwa nyumbani, iliishtua Wydad Casablanca kwa kuichapa bao 1-0, Al Hilal ikatoka sare ya bao 1-1 na Rivers United huko Nigeria, Petro Atletico ikalazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini na Otoho ya Congo huku Esperance ikitoka sare tasa ugenini na Al Ittihad ya Libya.

Simba sio tu inatambia kuzizidi kete timu hizo tajiri zaidi yake Afrika, bali kingine kinachowafanya watembee kifua mbele ni historia na rekodi nzuri ya ubabe dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika pindi inapocheza nazo ikiwa nyumbani ambazo zinawapa matumaini na imani kubwa kwamba wameshamaliza kazi kule Botswana na kutinga makundi ni suala la muda tu.

Katika mechi 10 zilizopita, Simba dhidi ya klabu za Kusini mwa Afrika, imeibuka na ushindi mara nane, kutoka sare moja na kupoteza mbili, imefunga jumla ya mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12.

Akizungumzia ushindi wa ugenini Gomes alisema; “Unapocheza ugenini siyo lazima kucheza soka la kuvutia badala yake unatakiwa kucheza kwa nidhamu ya kujilinda na kutumia nafasi unazopata kama wachezaji wangu walichofanya , nawapongeza sana kwa hilo.

“Tuliwatazama Galaxy kupitia mkanda wa video tukawaona wana shida kwenye mipira kona na ya kutenga hivyo tukatumia mapungufu yao kupata mabao,” amesema Gomes ambaye ni raia wa Ufaransa.

Alisisitiza kuwa kama ni pasi na mbwembwe zingine watazifanya Dar es Salaam wakishafuzu makundi.

Kocha wa Jwaneng Galaxy, Morena Ramoreboli alisema wana imani ya kupata ushindi hapa Dar es Salaam kwani Simba walibebwa katika mechi ya juzi

Ivo Mapunda staa wa zamani wa Simba alisema: “Simba wamecheza vizuri mashindano haya yanatizama matokeo sio namna ya uchezaji. Tuwaheshimu kwa kuwa wao ndio ngazi ya wengine kupandia.”