Simba SC yafyeka mastaa watatu

 Said Mohammed 'Nduda'

Muktasari:

  • Nyota watatu wa Simba Said Mohammed 'Nduda', Marcel Kaheza na Mohammed Rashid huenda wasiwe katika kikosi cha timu hiyo mara dirisha dogo la usajili kufunguliwa.
  • Mastaa hao ambao Kaheza na Rashid walisajiliwa mwanzo wa  msimu lakini wameshindwa kupata nafasi ya kucheza wakati Nduda nae msimu mmoja na nusu amecheza mechi moja wakatolewa kwa mkopo.

KUELEKEA katika dirisha dogo la usajili ambalo litafunguliwa Novemba 15 mastaa watatu wa Simba wamekubali yaishe na muda wowote kuanzia sasa watatolewa kwa mkopo kwenda kuzitumikia klabu nyingine.

Nyota hao ni Mohammed Rashid, ambaye alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea klabu ya Tanzania Prison ambapo msimu uliopita alimaliza ligi akiwa amefungia mabao kumi.

Tangu ametua Simba Rashid hajacheza hata mechi moja ya ligi ingawa alianza vizuri kwa kuonesha kiwango katika mashindano ya SportPesa na Kagame Cup, ambapo alifunga bao katika hatua ya makundi.

Marcel Kaheza, ambaye alisajiliwa na Simba mwanzo wa msimu akitokea Majimaji huku alikuwa nyota baada ya kumaliza msimu akiifungia timu yake mabao 12 licha ya kwamba timu hiyo ilishuka daraja.

Said Mohammed ‘Nduda’ naye ni miongoni mwa nyota ambao watatolewa kwa mkopo na kinachosubiliwa ni muda kufika ili kulitimiza hilo kwani, msimu mmoja na nusu aliokuwa katika kikosi cha Simba amecheza mechi moja tu dhidi ya Kagera Sugar msimu uliopita.

Rashid alisema tayari nimekubaliana na kocha kwamba nikatafute nafasi ya kucheza kutokana na ambao nacheza nao hapa katika nafasi moja watanipa muda mdogo wa kucheza.

“Nimekubaliana naye na ameniambia kama nitafanya vizuri huko ambapo nitakwenda nafasi ya kurudi hapa ipo wazi,” alisema Rashid ambaye anawindwa na Alliance, Mwadui, Prison na KMC ambao wanapewa nafasi kubwa ya kumnasa nyota huyo.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema katika kikosi chake nyota wote wanauwezo ila wale ambao hawajapata nafasi ya kutumika ni kutokana na changamoto ya kuwania nafasi ya kucheza.

“Changamoto ya kuwania nafasi ya kucheza ni kubwa mno katika timu yangu na haswa wale wachezaji ambao, wanapata nafasi ya kucheza kama wapo tayari nitawaruhusu lakini kama watafanya vizuri nafasi ya kurudi ipo wazi,” alisema Aussems.