Simba Queens, Yanga kinawaka leo

Summary

  • Timu hizo mbili ambazo kila mmoja inapambana kubeba ubingwa msimu huu, huku bingwa mtetezi Simba akijaribu kutetea nafasi yake huku hadi sasa wakiwa kileleni kwa pointi 26, nne mbele ya Yanga.

LEO kutakuwa na mtifuano mkali wakati mastaa wa Derby ya Kariakoo kwa upande wa wanawake(WPL), Simba Queens na Yanga Princess watakapokuwa uwanjani wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakitafuta ushindi muhimu.

Timu hizo mbili ambazo kila mmoja inapambana kubeba ubingwa msimu huu, huku bingwa mtetezi Simba akijaribu kutetea nafasi yake huku hadi sasa wakiwa kileleni kwa pointi 26, nne mbele ya Yanga.

Nahodha wa kikosi cha Yanga, Amina Ally amesema wanafahamu ubora wa timu pinzani hivyo wamefanya maandalizi ili kujiandaa na mchezo huo muhimu.

Alisema wamefanya juhudi zote kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu na kuongeza kuwa hakuna ugumu wowote.

"Tunajua umuhimu wa Derby, tunahitaji sana hizo pointi tatu lakini hii mechi kubwa na inahitaji kupambana ili kushinda na kuipa heshima timu yetu sasa hivi kila mchezaji akili na nguvu zote tumezielekezea huko,". Alisema Amina.

Kwa upande wa Kocha wa kikosi cha Simba Queens, Charles Lukula amesema mpaka sasa hajapokea taarifa ya majeruhi hata mmoja hivyo maandalizi yako vizuri kuwakabili Yanga.

"Tunaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wetu tunafahamu ni mgumu lakini tutapambana ndani ya dakika 90 kuhakikisha tunapata ushindi kila mechi huwa nawaambia wachezaji wangu ni fainali na hii pia ni fainali kwao". Alisema Lukula.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, timu hizo zilifanikiwa kutoka sare ya bao 1-1.