Simba noma! Yanga yaporwa staa hotelini, Azam wabaki na mkataba wao WhatsApp

SIMBA haina masikhara kabisa na maandalizi ya msimu ujao. Baada ya kufika hatua ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakibakisha hatua chache kutwaa taji la Ligi Kuu Bara (VPL), Simba sasa imehamishia hasira zake katika usajili mpya.

Taarifa za kuaminika ambazo Mwanaspoti imezipata ni Simba imemdaka juu ya kwa juu beki Charles Edward Manyama ambaye tayari alishafanya mazungumzo na Yanga akisubiri tu kusaini mkataba.

Manyama ambaye ametamba na Namungo FC kabla ya kutua Ruvu Shooting katika dirisha dogo amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuwatumikia mabingwa hao mara 20 wa VPL.

Beki huyo aliyewahi kucheza Yanga kwa mwaka mmoja msimu wa 2014/15, amekuwa katika kiwango bora tangu msimu uliopita na kupata nafasi katika kikosi cha Taifa Stars.Inadaiwa baadhi ya mabosi wa Yanga wapo jirani na Kambi ya Taifa Stars wakihaha kumalizana na beki huyo, lakini kumbe Simba walishamuwahi na kumsaini mapema.

“Yanga walikwenda mpaka hotelini wakiwa na mkataba na sehemu ya fedha lakini mchezaji akawazuga kwa vile muda mfupi uliopita Simba walishashtukia dili na kumalizana nae juu kwa juu.

“Halafu huwezi kuamini Manyama kabla hajamalizana na Simba alichukua ushauri kwa (anamtaja staa wa zamani wa Yanga) akamwambia achana na hizo Yanga na Azam nenda Simba kuna maisha,” kiongozi mmoja makini wa Simba aliidokeza Mwanaspoti jana Jijini Dar es Salaam.

Mbali na Yanga, Manyama pia alikuwa akiwaniwa na Azam FC ambayo ilikuwa tayari kumpa mkataba mnono, lakini ameipiga chini dili hiyo na kuwaachana na mkataba wao kwenye WhatsApp.

Kusainiwa kwa Manyama kunamaanisha vita ya nafasi sasa inakwenda kuibuka katika beki ya kushoto ya Simba ambayo imeshikwa muda mrefu na nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Zimbwe JR’.

Manyama alikuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha kwanza cha Stars kilichokwenda Chan ambapo Zimbwe JR aliachwa.

Hata hivyo bado hatma ya beki mwingine, Gadiel Michael haijafahamika kama ataachwa ama kuongezewa mkataba klabuni hapo lakini ni uhakika sasa Simba imeshamalizana na beki huyo mtaalam wa mashuti ya mbali.