Simba ni pasi mbili bao

KIKOSI cha Simba leo jioni kimefanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran, Dar es Salaam na kujinoa kwa mazoezi mbalimbali huku zoezi la kupiga pasi mbili na kufunga likionekana kuwa la kuvutia zaidi.

Timu hiyo inayojiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika leo ilifika uwanjani hapo saa kwa basi kubwa la timu na kuanza rasmi mazoezi saa 10:20 jioni.

Walianza kwa kunyoosha viungo na kuruka koni, zoezi ambalo lilidumu kwa dakika 15, wakati huo makipa watano wa klabu hiyo Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salim na Ahmed Feruz wakiendelea na mazoezi yao chini ya kocha wa makipa Milton Nienov.

Baada ya hapo kocha mkuu wa Simba Didier Gomes aligawa timu nne ambazo zilicheza kama mechi katika magoli madogo yaliyowekwa kwenye kila nusu ya uwanja.

Katika mechi hizo, Gomes na makocha wasaidizi wake, Seleman Matola na Thierry Hitimana walielekeza wachezaji wote kupiga pasi mbili kisha kufunga ambapo katika zoezi hilo Kibu Denis, John Bocco, Ibrahim Ajib, Yusuph Mhilu na Jimmyson Mwanuke walionekana kufunga sana kwa timu zao.

Baada ya hapo, makocha hao waligawa timu mbili na kucheza kama mechi uwanja mzima ambapo timu ya kwanza ilikuwa na wachezaji Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Sadio Kanoute, Hassan Dilunga, Rally Bwalya, John Bocco na Benard Morrison.

Kikosi cha pili kilikuwa na Ally Salim, Gadiel Michael, Israel Mwenda, Hennoc Inonga, Joash Onyango, Jonas Mkude, Ibrahim Ajib, Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni, Jimmyson Mwanuke na Kibu Denis.

Zoezi hilo lilidumu kama kwa dakika 20 hivi huku na kumalizika kwa bao 1-0, la timu ya pili likifungwa na Kibu Denis kwa kumchambua kiufundi Aishi Manula.

Baada ya hapo zoezi lilibadilika na kuanza kujifua kwenye kucheza mipira ya kona ambapo mabeki na viungo wakabaji walikuwa wakikaba huku viungo washambuliaji na mastraika wakifunga zoezi ambalo lilifanyika kwa dakika 15 kisha kumalizika huku kila mmoja akitimiza wajibu wake.

Dakika hizo 15 zilipomalizika wachezaji wote walikutana katikati ya Uwanja na kuzungumza kwa muda mfupi kisha kupanda basi na kuondoka.

Wachezaji waliohudhuria mazoezi ya leo ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salim, Jeremiah Kisubi, Ahmed Feruz, Israel Mwenda, Shomary Kapombe, Mohamed Mohamed, Gadiel Michael, Joash Onyango, Kennedy Juma, Pascal Wawa na Henoc Inonga.

Wengine ni Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Taddeo Lwanga, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, AbdulSamad Kassim, Rally Bwalya, Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga, Benard Morrison, Yusuph Mhilu,  Jimmyson Mwanuke, John Bocco na Kibu Denis.