Prime
Simba kumshusha kiungo aliyemkaba Cristiano Ronaldo

SIMBA hii sasa sifa! Mabosi wa klabu hiyo kongwe ambayo usiku wa jana ilikuwa inamalizana na APR katika mechi ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2004, wameonyesha hawataki utani kwenye dirisha dogo la usajili, baada ya kuhamishia rada zao kwa kiungo Msenegali Babacar Sarr.
Tulia kwanza. Simba ilianza kumtambulisha Saleh Masoud Karabaka. Kabla yake ilielezwa imeshampa mkataba winga kutoka Mtibwa Sugar, Ladack Chasambi na winga wa Tanzania Prisons, Edwin Balua.
Juzi usiku ikamshusha kiungo mshambuliaji nyota kutoka Zimbabwe, Michael Charamba kutoka Chicken Inn ambaye jana ilikuwa inamalizana naye jijini Dar es Salaam kabla ya kumpa mkataba.
Sasa kama ulikuwa unadhani kazi imeisha, basi pole yako, kwani mabosi hao wamemgeukia kiungo mkabaji anayejua boli kutoka Senegal, Babacar Sarr aliyewahi kumkaba Cristiano Ronaldo wa Al Nassr katika mechi za michuano ya Klabu Bingwa ya Nchi za Kiarabu iliyopigwa Julai 31, mwaka jana wakati akiichezea US Monastir ya Tunisia iliyocheza na Yanga msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mechi hiyo, Al Nassr ilishinda mabao 4-1 na ndio iliyobeba taji ikiifunga Al Hilal.
Kiungo huyo mkabaji anayetumia zaidi mguu wa kulia, mwenye umri wa miaka 26 jina lake lipo mezani kwa mabosi wa Simba wakimpigia hesabu za kumsajili, lakini wakisubiri uamuzi wa kocha mkuu, Abdelhak Benchikha ambaye naye alikuwa na jina la Eric Mbongossoum ili kuamua nani abebwe kati yao.
Utamu ni kwamba kwa sasa hana timu tangu alipomaliza mkataba na Monastir, Novemba mwishoni mwa mwaka jana, hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kula shavu kama mambo yatakwenda freshi.
Benchikha amewaangiza mabosi wa Simba kuletewa kiungo wa chini atakayeweza kufanya kazi nyingi na kuituliza timu baada ya waliopo kama Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute na Fabrice Ngoma kushindwa kumpa anachotaka licha ya kazi nzuri wanayofanya kikosini kwa sasa.
Mbali na Sarr na Mbongossoum ambaye ni raia wa Chad, mezani kwa mabosi wa Simba pia kuna jina la kiungo Mkongo, Mike Miche aliyeongezwa na viongozi kumpa nafasi kocha kuchagua amtakaye.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa uamuzi wa mwisho upo ndani ya saa 48 kuanzia leo ili kupitishwa kwa jina moja na wale watakaoshindwa kupenya wataachana nao mazima.
Raia huyo wa Senegal mwenye urefu wa mita 1.83 alizaliwa Julai 24, 1997 katika mji wa Thies, Senegal na amewahi kukipiga kwenye timu za Wallydann, AS Pikine, Mbour PC na Teungueth zote za Senegal kabla ya kutua Olympique Beja aliyotwaa nayo taji la Kombe la Tunisia msimu uliopita kabla ya kusajiliwa US Monastir aliyoichezea msimu huu kwa nusu msimu mechi saba na kufunga bao moja.
Inaelezwa Benchikha ametaka kuletewa haraka kiungo wa aina hiyo atakayekuja kutuliza eneo la kiungo mkabaji akichukizwa na hatua ya ukuta wake kuruhusu mabao mara kwa mara.
Bado mabosi wa Simba wanapambana kumshawishi Sarr ambaye inaonyesha anahitaji dau kubwa la usajili.
“Tunazungumza naye kama tutakubaliana tutafanya. Uamuzi huu wote tunamshirilisha na kocha (Benchikha) ili tuamue kwa pamoja,” alisema bosi mmoja wa wa juu wa Simba.
“Tunatakiwa kusajili kiungo mkabaji haraka. Kuna mambo kocha (Benchikha) hayafurahii kwenye eneo la kiungo mkabaji ndio maana kumekuwa na presha kubwa ya kumpata mtu wa aina hii.”
Simba inayoshiriki michuano ya kimataifa kama itampata mchezaji huyo, basi itakuwa imepata dodo kwenye mwarobaini kwani kwa sheria za CAF anaruhusiwa kucheza mashindano hayo.