Simba ishindwe yenyewe CAF

Muktasari:

  • Simba itacheza mchezo huo wa kwanza wa Kundi C ikianza msako wa tiketi ya robo fainali ya michuano hiyo, huku mwamuzi wa kati akiwa ni Mohamed Maarouf Eid Mansour kutoka Misri ambaye amewahi kuichezesha mechi za timu hizo zote.

SIMBA ishindwe yenyewe tu kwa Asec Mimosas baada ya kuangukia mikono salama kwa kupangiwa mwamuzi mwenye rekodi mbaya dhidi ya wapinzani wao katika mchezo wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Kwa Mkapa siku ya Novemba 25.

Simba itacheza mchezo huo wa kwanza wa Kundi C ikianza msako wa tiketi ya robo fainali ya michuano hiyo, huku mwamuzi wa kati akiwa ni Mohamed Maarouf Eid Mansour kutoka Misri ambaye amewahi kuichezesha mechi za timu hizo zote.

Awali, alikuwa mwamuzi wa akiba Simba ilipoichapa Horoya kwa Mkapa kwa mabao 7-0 Machi 18, 2023 pia aliichezesha tena katika Kombe la Shirikisho hatua ya mtoano Julai 18, 2018 dhidi ya Raja Casablanca na kumchapa kipa wa Asec, Abdoul Karim Cisse, kadi nyekundu katika dakika ya 68.

Mechi hiyo iliyochezwa Julai 18, 2018 ilimalizika kwa Asec kufungwa 1-0, shukrani kwa bao la mshambuliaji Mahmoud Benhalib aliyeuweka mpira kambani katika dakika ya 74 na waliporudiana Raja alishinda tena nyumbani kwa mabao 4-0.

Licha ya rekodi hiyo, Maarouf katika mechi 46 alizowahi kuchezesha katika mashindano yote ametoa jumla ya kadi za njano 207 na nyekundu 9 katika mashindano yote aliyosimamia.

Mwamuzi huyo aliwahi kutoa kadi za njano 10 kwenye mechi moja dhidi ya Ismaily vs Al Masry ya ligi ya Misri Aprili 7 2021.

Mwamuzi huyo atasaidiwa na Samir Saad na Youssef Elbosaty na mwamuzi wa mezani Mahmoudy Mosa wote kutoka Misri.

Kamishna wa mchezo huo ni Francis Oliele, muangalizi wa marefa Sylvester Kirwa wote kutoka Kenya na kwamba Asec ikitarajiwa kuja nchini na watu takribani 31.