Simba: Hizi ndo zetu

Nahodha wa klabu ya Simba, Nicholas Nyagawa akinyanyua juu kombe la ubingwa wa soka wa Tanzania bara walilokabidhiwa jana baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi kuu dhidi ya timu ya Yanga kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam , Simba ilishinda kwa 4-0
OLIVER ALBERT MASHABIKI wa Simba walikuwa wakiimba "Hizi ndo zetu," huku wakikimbia katika barabara mbalimbali za jijini Dar es Salaam. Simba imedhihirihisha msemo maarufu wa Kiswahili `wa mbili havai moja' baada ya kupaka rangi ubingwa wake kwa kuwaliza wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 4-3 kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Si tu imetwaa ubingwa bali imewagaragaza wapinzani wake wa jadi mara mbili kwenye ligi msimu huu na kudhihirisha kuwa huu ni mwaka wao kwani licha ya kutwaa ubingwa mapema bado ilikuwa na deni kwa mashabiki wake, nalo ni kuifunga Yanga. Kwa mashabiki wake, ubingwa usingekuwa mtamu bila ya kutoa kipigo kwa Yanga, ambacho kile cha jana kilikuwa cha pili baada ya kuishinda 1-0 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Oktoba 31, mwaka jana kwa bao la Mussa Hassan Mgosi. Pia Simba imepalilia njia ya kuweka rekodi mpya ya soka ya kutopoteza mechi kwenye ligi tangu mfumo wa kucheza nyumbani na ugenini ulipoanzishwa mwaka 1982. Isipofungwa na Mtibwa kwenye mechi ya mwisho basi itaandika historia kwenye soka la Tanzania ingawa tayari imeweka rekodi ya kutwaa ubingwa bila ya kupoteza mchezo. Kadi zatembea Mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mashabiki wa wastani pengine kutokana na mvua zinazonyesha mfululizo jijini Dar es Salaam, ulifanana na dhana nzima ya upinzani ya jadi baina ya timu hizo mbili kutokana na kukamiana na kucheza rafu za hapa na pale na Yanga kujikuta ikimaliza mchezo na wachezaji tisa wakati Simba ilibakiwa na watu 10. Mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akrama wa Mwanza alikuwa mkali na hakuwa na aibu kutoa kadi, na wa kwanza kuonja alikuwa beki wa Yanga, Wisdomu Ndlovu dakika ya 57 akifuatiwa na Amir Maftah wa Yanga dakika ya 86 kabla ya Hillary Echessa wa Simba kupewa dakika ya 92. Ushirikina Kama kawaida mchezo huo ulikuwa umegubikwa na imani za kishirikina kwa mfano njiwa mweusi alipoingia uwanjani mara baada ya Mussa Hassan 'Mgosi' alipofungia timu yake bao la pili na kiungo wa Yanga, Athumani Chuji kumpiga mateke lakini hakutoka hadi alipotolewa na mmoja ya watu aliyekuwa amekaa benchi la Simba. Pia kuna njiwa mweupe alirushwa kutokea upande wa Yanga baada ya timu hiyo kusawazisha bao, lakini aliishiwa nguvu pembeni ya uwanja na kuchukuliwa na shabiki wa Yanga. Mgosi akaribia kiatu cha dhahabu Mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi alikuwa shujaa kwa timu yake kutokana na kuzamisha mabao mawili katika mchezo huo na kuongoza kwa ufungaji wa ligi baada ya kufikisha mabao 16. Anawazidi kwa mabao mawili, John Boko wa Azam na Mrisho Ngassa wa Yanga, ambaye alifichwa na mabeki wa Simba kiasi pengine kusahau washambuliaji wengine kitendo ambacho kililalamikiwa na Kocha wa muda wa Simba, Selemani Matola, ambaye alikiri kuwa akili ya mabeki wake ilikuwa kwa Ngassa kiasi cha kusahau washambuliaji wengine. Karamu ya mabao Matokeo ya mchezo huo, yalidhihirisha kuwa timu zote mbili zilikuwa na uchu mkubwa wa ushindi tofauti na kawaida ya timu hizo kucheza kwa hadhari kubwa. Ni nadra kuona timu hizo zikifungana mabao mengi kwa sababu mara ya mwisho hali hiyo ilitokea mwaka 1996 wakati timu hizo mbili zilipofungana mabao 4-4 mjini Arusha kwenye mechi ya kufunga Ligi Kuu Tanzania Bara. Simba iliyofikisha pointi 59, ilionekana imepania kulinda heshima jana kwa kupata bao mapema dakika ya tatu lililozamishwa kimiani na Uhuru Selemani kwa shuti kali la pembeni baada ya uzembe wa beki wa Yanga, Maftah. Kipa wa Yanga, Obren Curkovic alidhani Uhuru angetoa pasi hivyo akatoka kidogo langoni, lakini Uhuru akapiga shuti ambalo lilikwenda moja kwa moja wavuni. Baada ya hapo, Yanga ilicharuka na kuisakama Simba vikali na `Chuji' aliisawazishia Yanga dakika ya 31 kufuatia kizaizai kilichosababishwa na faulo ya Abdi Kassim, ambaye shuti lake lilitemwa na kipa wa Simba, Juma Kaseja lakini Boniface Ambani akapiga shuti jingine likapanguliwa tena na Kaseja aliyekuwa chini na hivyo Chuji kuzamisha mpira wavuni kirahisi. Wababe hao walijikuta wakienda mapumziko wakiwa 1-1, lakini kipindi cha pili matokeo hayo yalibadilika. Kocha wa Yanga, Kostadin Papic alifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa Nurdin Bakari na kumuingiza Godfrey Bonny, kitendo kilichoshangiliwa na mashabiki wa Yanga waliokuwa hawajaridhishwa na kiwango cha Nurdin. Yanga ilikianza kipindi hicho kwa kasi na Ambani itabidi ajilaumu kwani dakika ya 46 alipoteza nafasi nzuri akiwa yeye na Kaseja baada ya pasi nzuri ya Mrisho Ngassa. Simba iliyokuwa bila ya kocha wake Patrick Phiri, ambaye anauguza mtoto wake nchini Zambia na kuwa chini ya nahodha wake wa zamani, Selemani Matola na Amri Said, iliamua kuongeza nguvu kwa kuwatoa Mohamed Banka na Michael Baraza na wakaingia Juma Nyosso na Emmanuel Okwi, ambao waliongeza uhai. Yanga nao walimwingiza Stephen Bengo badala ya Kiggi Makassy. Mussa Hassan `Mgosi' aliifungia Simba bao la pili dakika ya 53 baada ya kuwazidi mbio mabeki wa Yanga na kudokoa mpira uliomshinda kipa wa Yanga Obren Cuckovic, ambaye alijikuta akienda chini. Yanga ilipata pigo baada ya Ndlovu kutolewa kwa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano hivyo kuwa nyekundu baada ya kumkanyaga Nico Nyagawa wa Simba dakika ya 57 . Kufuatia hali hiyo ingetegemewa Yanga wangefanya mabadiliko kwenye safu ya ulinzi lakini tofauti na mawazo ya wengi, Papic, ambaye falsafa yake ni soka la kushambulia alimtoa Ambani na kumwingiza Jerry Tegete. Tegete hakumwangusha Papic kwani aliisawazishia Yanga baada ya kuunganisha `kiulaini' pasi ya Kassim aliyewachambua mabeki wa Simba dakika ya 67. Mgosi aliongeza bao la tatu la Simba dakika ya 73 baada ya kuunganisha kwa kichwa cha ufundi mkubwa krosi ya Okwi kutoka kwenye winga ya kushoto. Yanga ilijikuta ikibakiwa na wachezaji tisa baada ya Maftah naye dakika ya 86 kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa Juma Nyosso wa Simba. Pamoja na kucheza pungufu, Yanga haikukata tamaa bali iliendelea kuisakama Simba na kujipatia bao la tatu dakika mbili baadaye kwa penalti iliyofungwa na Tegete, ambaye shuti lake lilijaa wavuni licha ya kufuatwa na Kaseja aliyegusa mpira huo. Mwamuzi alitoa penalti hiyo baada ya Bengo kuangushwa kwenye eneo la hatari na Kaseja mwenyewe. Kiungo wa Simba, Echessa alifunga karamu ya mabao dakika ya 90 kwa shuti kali kufuatia pasi maridadi ya Uhuru. Echessa aliyekuwa na kadi ya njano alishangilia mpaka kwa mashabiki na kuvua jezi yake na aliporudi uwanjani akajikuta akipewa kadi ya pili hivyo kuwa nyekundu. Makocha Papic, ambaye ana uzoefu mkubwa na mechi za wapinzani wakubwa wa jadi barani Afrika kutokana kuzinoa Orlando Pirates na Kaizer Chiefs na Hearts of Oak ya Ghana yenye utani wa jadi na Asante Kotoko, alilalamikia kadi nyekundu ya Ndlovu na kudai haikuwa halali na kuongeza kutolewa kwa Maftah kuliidhoofisha zaidi timu yake. Aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kufunga licha ya kucheza pungufu katika mchezo huo mgumu. Matola alieleza kufurahishwa na ushindi wa timu yake lakini alilaumu mabeki wake kwa kuzembea na kutoa mwanya kwa Yanga kusawazisha mara matatu. "Mabeki wangu akili yao ilikuwa kwa Mrisho Ngassa na kusahau watu wengine na kutoa mwanya kwa Yanga kufunga mabao matatu licha ya kucheza pungufu kwa muda mwingi," aliongeza Matola, ambaye alikuwa kiungo mahiri wa timu hiyo kwenye enzi yake. Simba: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Juma Jabu/ Ulimboka Mwakingwe,Kelvin Yondan, Joseph Owino, Mohamed Banka/ Juma Nyoso, Nico Nyagawa, Hilary Echesa, Uhuru Suleiman, Mike Baraza/ Emanuel Okwi na Mussa Hassan Mgosi. YangaK Obren Curkovic, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah, Nadir Haroub Canavaro, Wisdom Ndlovu, Athuman Iddi Chuji, Kigi Makasy/ Steven Bengo, Abdi Kassim, Nurdin Bakari/Godfrey Bony, Boniface Ambani/ Jerry Tegete na Mrisho Ngassa.