Simba hii haijawahi kutokea kabisa

Muktasari:

  • Kikosi hicho sio kinashtua pengine labda haichezi vizuri, hapana! Simba bado ina kikosi imara na inacheza vizuri kama ilivyocheza soka tamu pambano la dabi ililopoteza mabao 2-1 na kuendelea kusalia nafasi ya tatu na pointi 46 baada ya mechi 21.

ACHANA na kipigo ilichopewa na Yanga katika Kariakoo Dabi iliyopigwa juzi Kwa Mkapa, ukweli ni Simba ya sasa inashtua.

Kikosi hicho sio kinashtua pengine labda haichezi vizuri, hapana! Simba bado ina kikosi imara na inacheza vizuri kama ilivyocheza soka tamu pambano la dabi ililopoteza mabao 2-1 na kuendelea kusalia nafasi ya tatu na pointi 46 baada ya mechi 21.

Simba ya msimu huu imeshtua kwa namna ukuta wake ulivyo mwepesi kuliko kipindi chote ndani ya misimu 10 iliyopita na umekuwa laini sana na kuruhusu mabao kiwango cha kuwashtua hadi mashabiki na hata kocha wa klabu hiyo kongwe nchini.

Unaweza usiamini, lakini ndio ukweli ulivyo. Simba hii ya Abdelhak Benchikha katika kipigo cha juzi kilichokuwa cha tatu kwa msimu huu, tayari imeruhusu mabao 21 katika mechi 21 tu. Hii ikiwa na maana kila mechi timu hiyo imeruhusu bao moja, kitu ambacho hakijawahi kutokea katika misimu mingine tisa iliyopita.

Kikosi hicho ukuta wake umekuwa ukilindwa na makipa Ally Salim, Aishi Manula na Ayoub Lakred, huku mabeki wa pembeni wa kongwe Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Eneo hilo la pembeni pia lina David Kameta ‘Duchu’ na Israel Patrick Mwenda, huku beki ya kati inayounda ukuta huo ambao awali ulibatizwa jina la Ukuta wa Yeriko, una vichwa kama Henock Inonga, Fondoh Che Malone, Kennedy Juma na Hussein Kazi.

Ukuta huo unalindwa na viungo wa ukabaji akiwamo Babacar Sarr, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute ambao wamekuwa wakipokezana na kuna wakati wameonekana kukosa mizani sawa na eneo la nyuma.

Rekodi za msimu huu zinaonyesha katika mechi 21 ilizocheza Simba hadi sasa katika Ligi Kuu Bara, 13 kati ya hizo imeruhusu mabao, huku michezo nane tu ndio ilikomaa bila kufungwa bao lolote ikiwa ni rekodi mbovu zaidi  kwa kikosi hicho cha Msimbazi.

Simba imeruhusu mabao katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, iliyoshinda 4-2 ugenini, kisha ikashinda 3-1 mbele ya Tanzania Prisons na 2-1 dhidi ya Singida FG zote pia zikiwa za ugenini, lakini iliporudi nyumbani ilishinda 2-1 dhidi ya Ihefu kabla ya kucharazwa 5-1 na Yanga na kutoka sare ya 1-1 na Namungo na ile ya 2-2 dhidi ya KMC iliyokuwa wenyeji wa pambano hilo.

Mechi nyingi ilizoruhusu bao ni dhidi ya Azam (1-1), ilipolala nyumbani 2-1 kwa Prisons, ikaenda kuifunga Coastal Union jijini Tanga kwa mabao 2-1 na kuifumua tena Singida FG kwa mabao 3-1 jijini Dar kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini mbele ya Ihefu na juzi kulala 2-1 kwa Yanga.

Mechi nane ambazo Simba ilikomaa bila ukuta wa timu hiyo kuruhusu bao lolote ni dhidi ya Dodoma Jiji (2-0), Coastal (3-0), Kagera Sugar (3-0), Mashujaa (1-0 na 2-0), Tabora United (4-0), Geita Gold (1-0) na JKT Tanzania (1-0).

Hali hiyo ni tofauti na misimu tisa iliyopita na ni msimu mmoja tu wa 2019-2020 iliruhusu idadi ya mabao kama hiyo ya 21, lakini kwa kucheza msimu mzima uliokuwa na mechi 38. Katika msimu huo Simba ilibeba ubingwa ikifunga pia mabao 78 na kufungwa 21, huku misimu mingine haikuwahi kufungwa idadi hiyo.

Msimu wa 2014-2015, Simba katika mechi 26 ilizocheza ilifunga mabao 38 na kufungwa 19, 2015-2016 iliruhusu mabao 17, lakini yenyewe ikifunga 45 katika mechi 30 za msimu mzima na ule wa 2016-2017 Simba ilifunga mabao 50 na kufungwa 17.

Msimu wa 2018-2019 Simba katika mechi 38 ilifunga mabao 77 na kufungwa 15, huku msimu wa 2020-2021 katika michezo 34 ilifunga 78 na kufungwa 14, ilihali msimu wa 2021-2022 katika mechi 30 ilifunga 41 na kuruhusu 14 na msimu wa uliopita ilifunga mabao 75 na kufungwa 17 kupitia michezo 30.


WASIKIE MAKOCHA

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amekiri udhaifu wa safu yao ya ulinzi kwa kikosi chao kuruhusu mabao mengi akisema bado kuna changamoto katika eneo lao la ulinzi lakini zipo hesabu za kwenda kurekebisha.

“Ni kweli tumeendelea kuruhusu mabao, sio takwimu nzuri kwa klabu kubwa kama Simba, ila hayo tumeyaona na ipo mikakati ya kwenda kufanya marekebisho zaidi,” alisema Matola mara baada ya pambano la juzi ilipolala kwa mara ya pili msimu huu mbele ya Yanga.

Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema matatizo ya Simba kuruhusu mabao yanajulikana na makosa hayo yanatokea kutokana na mabeki kukosa watu bora wanapocheza mbele yao kwenye safu ya kiungo.

“Ukiniambia Simba ina mabeki dhaifu nitakataa, sio kila wakati inaporuhusu mabao sana shida inakuwa ni mabeki wa kati, shida ya Simba bado kikosi hakijacheza kwa uwiano mzuri, bado timu haina viungo halisi wazito wanaoweza kucheza kwa ubora mbele ya mabeki wa kati,” alisema Robertinho aliyetimuliwa mara baada ya Simba kufungwa mabao 5-1 na Yanga katika Kariakoo Dabi ya Novemba 5 mwaka jana na kuongeza;

“Angalia watu waliokuja kucheza eneo hilo bado huoni wana uzito wa kupunguza mzigo mkubwa kwa mabeki wa kati, pia yapo makosa yanafanyika pembeni ya uwanja, Simba inahitaji wachezaji wenye akili kubwa katika kurudisha ubora wa kikosi.”

“Simba itahitaji muda, mambo hayatakiwi kufanyika kwa presha, timu itajengwa taratibu lakini nasisitiza ili wawe bora wanatakiwa kuwa watulivu kwenye maamuzi na sio kufanya mambo kwa kukimbizana, wanatakiwa kuwasikiliza makocha pia wakati wa kuleta wachezaji,” alifafanua Mbrazili huyo.