Simba Dar? Labda itokee tu

MASHABIKI wa Simba bado hawaamini kama walishindwa kutoka na ushindi  dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kama watasoma rekodi ya timu hiyo kwa mechi za nyumbani za CAF, basi wana kila sababu ya kuanza kuchekelea.

Simba imelazimisha sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Mjini Ndola, huku timu hiyo ikipoteza nafasi nyingi za kuifanya itoke na ushindi mnono, lakini bado ina dakika 90 za mchezo wa marudiano utakaopigwa Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku ikibebwa na rekodi tamu za nyumbani.

Mwanaspoti fukua fukunyua yake, imebaini Simba tangu iliporejea tena kwenye michuano ya CAF mwaka 2018, timu hiyo imechezea jumla ya mechi 26 ikiwa nyumbani zikiwamo 19 za Ligi ya Mabingwa na nyingine saba za Kombe la Shirikisho.

Katika mechi hizo 19 za Ligi ya Mabingwa, Simba imepoteza michezo miwili na kutoka sare mitatu, huku ikishinda 14 na jumla ya michezo hiyo timu hiyo imefunga mabao 41 na kuruhusu mabao 11 tu.

Michezo pekee ambao Simba ilipoteza ilikuwa ule wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2021-2022 mbele ya Jwaneg Galaxy ya Botswana iliyowafumua mabao 3-1 baada ya awali kushinda ugenini kwa mabao 2-0 na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini lililowabeba wapinzani wao, kisha ikalala 3-0 msimu uliopita kwenye hatua ya makundi mbele ya Raja Casablanca.

Mechi ilizotoka sare ni ile ya robo fainali ya msimu wa 2018-2019 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo ilikataa kuruhusu bao na kwenda kushinda ikiwa kwao kwa mabao 4-1, pia sare ya 1-1 iliyoing’oa mbele ya UD Songo ya Msumbiji katika raundi ya awali ya msimu wa 2019-2020 na suluhu dhidi ya Plateau United ya Nigeria kwenye raundi ya awali msimu wa 2020-2021.

Katika mechi saba za Kombe la Shirikisho, Simba haijapoteza mchezo wowote wa nyumbani zaidi ya kutoka sare moja tu ya 2-2 dhidi ya Al Masry katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo msimu wa 2018, huku nyingine sita zilizosalia ikitakata kwa kushinda na kufunga jumla ya mabao 19 na kufungwa mabao matatu tu, hii ikiwa na maana mchezo ujao dhidi ya Wazambia utakuwa ni wa 27 kwa michuano yote ya CAF.

Na kwa rekodi hiyo ya mechi ya nyumbani ni wazi mashabiki wa Simba wajiandae tu kuendelea kupata furaha, japokuwa Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema ni mechi ngumu, lakini analipanga jeshi lake ili kuhakikisha wanapata matokeo yatakayowavusha kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya tano.

Simba imefuzu katika hatua ya makundi ikiwamo ya 2013, 2018-2019, 2020-2021 na 2022-2023 kwa Ligi ya Mabingwa na 2021-2022 ya Shirikisho.