Siku 12 za moto Simba

Klabu ya Simba kutoka leo inakuwa imebakiza siku 12 za moto kwa ajili ya kujiandaa na kucheza mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa dhidi ya Asec Mimosas.

Simba itakuwa mwenyeji katika mchezo wa kwanza katika kundi B dhidi ya Asec utakaochezwa Novemba 25 mwaka huu kisha Disemba 2 itaenda nchini Afrika Kusini kucheza dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Wakati Simba ikiwa inatarajia kurejea kambini hivi karibuni baada ya mapumziko mafupi na sasa inajiandaa na mechi hiyo, inatakiwa kuwa na utulivu mkubwa wa maandalizi ya mchezo huu wa Ligi ya Mabingwa.

Timu hiyo ambayo imetoka kuachana na aliyekuwa kocha wao, Roberto Oliveira bado haijawa na utulivu kwani hadi sasa bado hakuna ambaye ametambulishwa kuwa kocha mpya kurithi mikoba ya Robertinho huku timu ikiwa ina mechi muhimu.

Benchi la ufundi kwa  sasa linaloongozwa na kaimu kocha mkuu Daniel Cadena akisaidiana na Seleman Matola ambao wana kazi kubwa ya kufanya ili kurejesha sura ya furaha kwa mashabiki zao.

Cadena na Matola jambo la kwanza inabidi wawasaulishe mastaa wao matokeo ya yuma dhidi ya Yanga ambayo walifungwa 5-1 na mchezo wao dhidi ya Namungo uliomalizika kwa sare 1-1 na akili iwe katika mechi hii.

Wakati huo huo wawili hao wana kazi ya ziada kutengeneza mbinu zao mpya kwa wachezaji wao ndani ya siku hizo ili iweze kuwasaidia katika kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya  Asec hapa nyumbani na mbaya zaidi hawana mechi yoyote ile ya Ligi Kuu hadi siku itakapokuwa na mchezo huo.

Huu ni wakati ambao Cadena na Matola anatakiwa atulie kwa umakini kwani wachezaji wengi alishawahi kufanya nao kazi hapo awali kabla ya kuondolewa katika timu hiyo na kupelekwa kwa vijana.


Simba pia Uongozi sambamba na benchi la ufundi wanatakiwa kuzuia presha kwa wachezaji na kutengeneza usawa sambamba na uaminifu ili kuhakikisha inapata matokeo.

Hakuna shaka upande wa kimataifa Simba inafanya vizuri kwani hata katika African Football League ikiwa chini ya Robertinho,   imecheza mechi mbili dhidi ya Al Ahly na haikufungwa baada ya kutoka sare nyumbani 2-2 na ugenini 1-1 kisha ikaondolewa kwenye mashindano hayo kwa kanuni ya bao la ugenini.

Lakini kabla ya mashindano hayo Simba ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ikiwa chini ya Robertinho baada ya kutoka sare ya jumla ya mabao 3-3 dhidi ya Power Dynamos baada ya timu hiyo mchezo wa kwanza uliochezwa Zambia kutoka sare 2-2 na hapa Tanzania kutoka 1-1.

Wadau wa soka wametaka timu hiyo kwa pamoja waungane kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo muhimu wa kwanza kwao katika hatua ya makundi.

Beki wa zamani Simba, Fikiri Magoso alikiri wazi kuna sehemu timu yake inafeli  lakini inabidi washikamane kuhakikisha wanavuka kipindi cha mpiti walichonacho.

"Simba tuna mitihani mikubwa lakini naomba tushikamane, ujue hata hapa kwenye makundi tumeingia kwa bahati kwa sababu tumekuwa watu wa kunyoosha mikono, Simba inafunga halafu inafungwa;

Akizungumzia uwepo wa Cadena na Matola alisema;"Wote hao wana kazi ngumu kwa sababu kiuhalisia kocha unahitaji ukae na timu wiki tatu au mwezi ili uweze kuingiza mfumo wao lakini kikubwa inabidi waungwe mkono."

Upande wa mshambuliaji wa zamani Simba,  Bakari Kigodeko alisema wachezaji na benchi la ufundi wanabidi wasahau matokeo ya nyuma na sasa akili yao iwe katika mchezo huo.

Kigodeko alisema hana shida na Simba kwenye mechi za kimataifa licha ya kutokuwa na ushindi lakini hilo halimfanyi akose imani nao.

"Kwenye Ligi ya Mabingwa Simba inakuwa ni tofauti kabisa na kwenye Ligi inavyocheza na hilo linajulikana hivyo imani yangu itafanya vizuri;

"Matola na yule mwingine (Cadena) wote ni wazuri hivyo bila shaka wakisaidiana kwa pamoja basi timu itapata matokeo."