Siku 10 tu, Pablo aliamsha

Kocha mkuu wa Simba Pablo Franco. Picha | Simba

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco akiwa na siku 10 tu tangu ajiunge na timu hiyo akitokea kwao Hispania leo anatarajiwa kuliamsha dude kwa kukiongoza kikosi chake katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting.

 Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza ni kama mtego kwake wa kuhakikisha anaing’arisha nyota yake au kuififisha mapema kwa mashabiki wa klabu hiyo kutokana na aina ya matokeo itakayopata kwa wapinzani wao hao wanajiita Barcelona ya Bongo.

Pablo aliyetua nchini Novemba 10, siku tatu tangu atangazwe na kutambulishwa na mabosi wake hao, bila ya shaka analazimika kuhakikisha timu yake inaibuka na ushindi leo, ili kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara, Yanga, pia ikiwa ni kuepuka kujiweka kwenye presha kubwa za mapema.

Licha ya kusimamia mazoezi ya timu hiyo kwa takribani siku saba tu, hakuna uwezekano mkubwa kwa Pablo kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake leo kukabiliana na Ruvu ambao ndio wenyeji wa mchezo na waliotoka kupoteza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Yanga kwa kulala 3-1.

Bila ya shaka Pablo ataendelea kutegemea msaada wa wasaidizi wake wawili, Hitimana Thiery na Selemani Matola ambao ndio waliosimamia timu hiyo mara baada ya kutemwa kwa kocha Didier Gomes.

Kwa upande mwingine ni mchezo ambao utampa picha halisi Pablo ya utimamu na uwezo wa kutafsiri mbinu wa wachezaji wake siku chache kabla ya mechi muhimu na ngumu nyumbani ya hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia itakayopigwa Nov 28.

Ruvu inaingia katika mchezo huo ikiwa na pigo la kumkosa kocha mkuu, Boniface Mkwasa anayetumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu na faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kutoa kauli zisizofaa kwa waamuzi wa mchezo wao uliopita dhidi ya Yanga.

Timu hiyo kwa leo itaongozwa na kocha msaidizi Rajab Nakuchema, ikiwa na kiu ya kutaka kuendeleza kile ilichokifanya msimu uliopita katika mechi ya awali kwa kuinyoa Simba 1-0 kabla ya kupasuka hapohapo Kirumba waliporudiana kwa mabao 3-0.

Simba itaikabili Ruvu ikiwa na nguvu kubwa iliyoipata sio tu kwa kuwa na kocha mpya bali urejeo wa viungo, Sadio Kanoute na Pape Sakho waliokuwa majeruhi.

Ni mechi ambayo inakutanisha timu mbili ambazo zinasumbuliwa na tatizo la ubutu katika safu ya ushambuliaji ambapo kila moja katika mechi tano zilizopita, imefunga mabao matatu tu.

Lakini utofauti unakuja katika uimara wa safu za ulinzi ambapo ile ya Simba inaonekana kuwa tishio zaidi kwani haijaruhusu bao lolote hadi sasa wakati Ruvu imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano, ikiwa ni wastani wa bao moja katika kila mchezo.

Simba inapaswa kuwa makini zaidi na Ruvu katika mashambulizi ya kushtukiza kwani timu hiyo imekuwa na hulka ya kupendelea kutumia mbinu hiyo pindi inapocheza dhidi ya Simba, Yanga ama Azam ambapo huwa inajaza idadi kubwa ya wachezaji katika eneo la kujilinda na kushambulia kwa kasi wanaponasa mpira.

Lakini kwa upande wa Ruvu nayo inatakiwa kuwa makini zaidi na mashambulizi ya kutokea pembeni ya uwanja na yale yatokanayo na mipira ya juu ambayo Simba ndio inaonekana kutumia mara kwa mara msimu huu.

Rekodi zinaonyesha katika mechi 10 zilizopita baina ya timu hizo, Simba imeonekana kufanya vyema zaidi ambapo imeibuka na ushindi mara nane, imetoka sare moja na Ruvu imeshinda mechi moja tu.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema anatamani kuona timu yake ikipata ushindi leo, kwa kuzingatia ni mchezo wake wa kwanza katika Ligi ya Tanzania.

“Ni mechi yangu ya kwanza natamani kupata matokeo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuendeleza ushindani,” alisema Pablo.

Ruvu kupitia nahodha wao, Renatus Ambrose imesema kupoteza kwao 3-1 dhidi ya Yanga isiwafanye Simba wajiamini kwamba watapata mteremko leo huku kocha msaidizi wa timu hiyo, Nakuchema alisema kukosekana kwa kocha mkuu Mkwasa haitawaathiri.

Mechi nyingine leo itakuwa mkoani Rukwa ambako wenyeji Prisons wataikaribisha Mbeya Kwanza wakati kule Moshi, Polisi Tanzania watakuwa wenyeji wa Coastal Union

Kocha wa Prisons, Shaban Kazumba alisema wamejipanga kuhakikisha wanashinda mechi ya leo.

“Hatujapata ushindi katika mechi tano zilizopita hivyo mechi hii tunatakiwa kushinda ili kuweka mambo sawa. Tunajua mechi itakuwa ngumu lakini tumejiandaa vilivyo,” alisema Kazumba.