Barbara: Subirini muone

Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez.

KIKOSI cha Simba jioni ya jana kiliondoka Dar es Salaam, kuelekea Mwanza kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba, huku Mtendaji Mkuu wake, Barbara Gonzalez akiwatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwamba mambo matamu yanakuja.

Barbara aliyefiwa na mama mzazi hivi karibuni, alisema wanasimba hawana haja ya kuwa na hofu yoyote na timu yao, kwani licha ya malengo yao ya kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika kukatiliwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana na kupoteza Ngao ya Jamii kwa Yanga bado wapo fiti.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barbara alisema katika kuonyesha kuwa Simba imejipanga kwelikweli kusahihisha makosa, wameamua kuimarisha benchi lao ufundi kwa kuleta mafundi wawili kutoka Hispania na kusisitiza wanaoibeza timu yao wasubiri, kwani hawataamini kitakachotokea.

Alisema kuonyesha walivyo siriazi msimu huu, ndio maana makocha wenye majina makubwa Afrika kama Lamine N’Diaye, Rolani Mokeana na Miguel Angel walishindwa kupata nafasi hiyo kutokana na kushindwa kufikia vigezo vyao walivyohitaji na kumchukua, Pablo Franco.

“Tutalipa benchi la ufundi nguvu katika kuhakikisha wanapata kila ambacho wanahitaji ili kuipa timu yetu mafanikio kama ambavyo tunatamani kuiona Simba inafika hapo,” alisema Barbara na kuongeza;

“Tumepoteza sehemu mbili, Ngao ya Jamii na Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kufuta machungu kama viongozi kushirikiana na wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki tukiwekeza nguvu ya kutosha kwanza kutetea mataji ya ndani,” alisema Barbara na kuongeza;

“Pia tupo Kombe la Shirikisho tunahitaji umakini mkubwa na wachezaji wetu wanaelewa hilo lengo kubwa ni kufika mbali katika mashindano haya ya kimataifa ambayo ni wawakilishi pekee kutoka Tanzania tumebakia.”

“Uongozi umejipanga kuwapatia na kuwapa nguvu benchi la ufundi na wachezaji kila ambacho wanahitaji tena kwa wakati. Muda huo huo tunaendelea kuboresha timu yetu kutoka na mapungufu ambayo tunayo,” alisema.

Aidha Barbara alisema kutokana na kiu kubwa aliyokuwa nayo kocha wao mpya katika mafanikio haswa kufundisha Afrika kwa mara ya kwanza wanaimani nae kubwa, huku akidokeza kwa sasa wanafanya mchakato wa kuleta Kocha wa Makipa kuchukua nafasi ya Mbrazili Milton Nienov.

“Bado tupo katika kuboresha benchi la ufundi ili kupata kile tunachohitaji na kuona hilo linakwenda vizuri tupo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mzuri mpya wa makipa,” alisema Barbara.