Shoji amejipata, asubiri simu ziite

New Content Item (1)
New Content Item (1)

BAADA ya kukosekana uwanjani kwa takribani misimu miwili, straika wa zamani wa Dodoma Jiji, Jimmy Shoji amerejea upya huku akisema yupo tayari kukiwasha popote msimu ujao.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu kadhaa ikiwamo Polisi Tanzania na Mbeya Kwanza, kwa sasa yupo jijini Mbeya akiendelea na mazoezi binafsi kujiweka fiti.

Straika huyo aliumia goti tangu raundi ya kwanza ya msimu uliopita wakati timu yake Dodoma Jiji ikimenyana dhidi ya KMC na kujikuta nje baada ya kufanyiwa operesheni na sasa ameonekana kuwa fiti.

Akizungumza baada ya mchezo wa kirafiki baina ya Football Family anayojifua nayo dhidi ya Prisons ulioisha kwa sare ya 2-2, Shoji alisema kwa sasa ameimarika na anasubiri msimu ujao kurejea rasmi uwanjani.

Nyota huyo ambaye alifunga bao kwenye mchezo huo, alisema kwa muda alioanza mazoezi hadi kufikia msimu ujao atakuwa amerejesha kiwango chake kwani maandalizi aliyonayo yanampa matumaini.

“Ni muda mrefu nimekuwa nje, lakini kwa sasa nimeimarika na ninaendelea na mazoezi binafsi ikiwamo mechi kama hizi kunipa utimamu, nasubiri msimu ujao kurudi uwanjani,” alisema straika huyo.

Mchezaji huyo mwenye kasi na mwili wa kazi uwanjani, alifafanua kwa sasa yuko huru kufanya mazungumzo na timu yoyote na hachagui bali ishu ya masilahi ndio itaamua.