Serikali yabariki rasimu ya Katiba Simba

KLABU ya Simba inajiandaa na mkutano mkuu utakaofanyika Jumapili ya wiki hii, huku Kamati ya Maboresho ya Katika ya klabu hiyo imeeleza mkachato wa kutekeleza agizo ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) umeenda vyema.

Simba imekwama kukamilisha mchakato wa mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo baada ya serikali kuitaka ifanye maboresho ya katiba na hivi karibuni uongozi  ulitangaza Kamati ya Maboresho ya Katiba hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Wakili  Hussein Kita ambaye jana ilitangaza kukamilisha kupokea maoni ya wanachama juu ya maboresho hayo na kuyafanyia kazi.

Kita amesema baada ya kupitia maoni ya wanachama wao kamati ilikutana kujadili na kutengeneza rasimu ya Katiba na kuipeleka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambayo imepitishwa na kupelekwa kwa wanachama kuipitia kabla ya kujadiliwa na mkutano mkuu utakaofanyika keshokutwa Jumapili.

Alisema, maelekezo ya maboresho hayo waliyapokea baada ya FCC kutoa maelekezo Rita na BMT ya kuwataka wayafanyie kazi ili mchakato wao wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ukamilike.

Kita aliyataja maeneo ambayo yalitakiwa kuboreshwa ni mamlaka ya uteuzi wa Bodi ya Wadhamini, nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ambayo kwa katiba ya sasa haisemi chochote, malengo ya Simba yaelezwe wazi, namna ya kupata kolamu ya wanachama kwenye mkutano mkuu, chombo cha Simba Sports Holding Company Limited ambacho ndicho mmiliki wa hisa, asilimia 99 za hisa kumilikiwa na Bodi ya Wadhamini na asilimia moja kumilikiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini.

"Tumekaa vikao vingi sana, lakini vikubwa vilikuwa vinne, awali tuliitwa na Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro kutuuliza kwanini mchakato wa uendeshaji wa klabu haukamiliki, tulimweleza sababu zilizotukwamisha kila tunapofanya jitihada. Waziri alishirikisha wadau wote Simba, FCC, Rita, TFF na BMT," alisema Kita na kuiongeza;

"Kwa mchakato utakamilika mara tu wanachama watakapitisha hii Rasimu ya Katiba kwenye mkutano mkuu, kwani BMT tumewapelekea na wametupa barua ya kuridhika na namna tulivyofanya kwa kufuata maelekezo yao, hivyo sasa ni jukumu la wanachama kuipitisha siku ya mkutano mkuu ingawa kikatiba tumewatumia kupitia matawi ili waipitie na siku hiyo tuweze kuijadili tu."

Wakili Kita alisema maboresho hayo yatakuwa na faida kwa pande zote mbili klabu na wanachama kwani yatasaidia kukamilisha mfumo wao wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ambayo umekwama kwa zaidi ya miaka mitano.

Simba kwa sasa ipo chini ya Bodi ya Wakurugenzi ambapo awali Mwenyekiti alikuwa ni Mohamed Dewji ambaye ni mwekezaji wa klabu hiyo, lakini sasa bodi ipo chini ya Salim Abdallah 'Try Again', huku Murtaza Mangungu akiwa Mwenyekiti wa klabu akichaguliwa na wanachama.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajuna kwa upande wake alisema; "Maboresho hayo yamechukuwa muda mrefu hadi hapo yalipofikia lakini Jumapili ndiyo itakuwa hitimisho kwa wanachama kuamua kuipitisha Rasimu hiyo. Hivyo mkutano mkuu ajenda kuwa itakuwa ni hiyo na kufautiwa na zingine."