Serikali kugharimia mashabiki wa Yanga kwenda Afrika Kusini

Muktasari:
- Mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Mamelodi Sundowns na Yanga utachezwa katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini, Aprili 5
Rais wa Yanga, Hersi Said ameishukuru Serikali kwa kukubali ombi la kuwasafirisha mashabiki 48 kwa ajili ya kwenda kuipa timu hiyo ushirikiano kwenye mchezo wa pili wa hatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi, utakaopigwa Afrika Kusini, Ijumaa wiki hii.
Hersi amesema alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa kuwaaga wanachama na mashabiki wanaosafiri kwenda Afrika Kusini katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani.
Yanga itashuka dimbani Aprili 5, ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia suluhu kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa nyumbani Jumamosi iliyopita na keshokutwa Jumatano wanaondoka kuifuata Mamelodi.
"Tunafahamu klabu yetu ina mchezo mwingine wa pili kule Afrika Kusini, hivyo uongozi umefanya jitihada za kupeleka ombi katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wetu Dk Damas Ndumbaro la kusafirisha mashabiki kwa njia ya basi na tunaishukuru wizara kwa kukubali ombi letu," amesema Hersi.
Amesema wizara itahudumia gharama zote za safari ya kwenda Afrika Kusini kwa wanachama na mashabiki 48 kuanzia nauli mpaka pesa ya kujikimu, hivyo wao kama viongozi wanaishukuru serikali.
“Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na Sh600,000 na tulipata watu 30. Niwahakikishie baada ya wizara kukubali kusafirisha wanachama na mashabiki wetu, zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe,” amesema.
“Niwatakie safari njema na nina imani safari yetu ya kurudi itakuwa nzuri kwa kuwa tutarudi tukiwa tayari tumeshafuzu hatua ya nusu fainali.”
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' alisema Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuwa sehemu ya mchango wa kuhakikisha timu hiyo inafanya vyema nchini Afrika Kusini.
"Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imekubali kugharamia safari hii kwa asilimia mia moja itakayowafanya mashabiki kindakindaki wa Yanga kuishangilia timu yao wakiwa uwanjani ikiwa ni sehemu ya kuonyesha ushirikiano wetu kwenye michezo nchini," alisema Mwana FA