Serengeti Girls tunawaamini

KUELEKEA mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia kati ya timu ya taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls dhidi ya Japan, wadau wa soka wamesema wana matumaini makubwa kuona timu hiyo ikianza vizuri.

Timu hiyo iliyopangwa kundi D pamoja na timu za Japan, Ufaransa na Canada inatarajia kuingia uwanjani leo Jumatano kuanzia saa 11:30 jioni kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru, Margao India.

Kocha wa Fountain Gate, Juma Masoud alisema; “Najua wanaenda kufanya vizuri hii inatokana na maandalizi waliyofanya kabla ya michuano hii, nimefuatilia sana katika kipindi chote walichokuwa kambini England naaamini tutafanya vizuri.”

Kocha huyo alitoa tahadhali kwa timu hiyo kuwa; “Licha ya timu hiyo kuonekana kuwa na uwezekano wa kufanya vizuri lakini wanatakiwa kuchukua taadhari hawatakiwi kuwadharau wapinzani wao.”

Kiraka wa zamani wa Simba, Yanga na Azam, Amri Kiemba alieleza; “Vijana wetu wapo vizuri na hata ukiwatazama namna wanapokuwa mazoezini wanaonekana wana moyo wa kutamani kupata matokeo mazuri hivyo sina shaka labda itokee bahati mbaya.”