Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serengeti Boys na fainali ya heshima, historia AFCON      


Timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kesho Jumanne kuanzia saa 4:00 usiku itakuwa uwanjani jijini Rabat, Morocco ikicheza fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri huo (AFCON U17) 2026.

Katika mchezo huo ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Hassan, Serengeti Boys itakabiliana na Senegal huku timu hizo mbili zikitanguliwa na mechi ya kuwania mshindi wa tatu baina ya wenyeji Morocco na Misri.

Serengeti Boys ilitinga hatua ya fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Misri baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare tasa.

Senegal iliingia hatua ya fainali baada ya kuichapa Morocco kwa mikwaju ya penalti 7-6 kufuatia dakika 90 za nusu fainali yao kumaliza kwa sare ya bao 1-1.


Ni heshima, historia

Kitendo tu cha kuingia hatua ya fainali ni heshima kwa timu hiyo kwani imekuwa timu ya taifa ya kwanza ya Tanzania kuingia katika fainali ya mashindano yaliyo chini ya Mataifa ya Afrika yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mafanikio makubwa yaliyowahi kufikiwa na timu za taifa za Tanzania katika fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake na wanaume ni yale ya timu ya wakubwa ya Wanaume kufika hatua ya 16 bora ya Fainali za Mataifa ya Afrika 2025.

Kiujumla itafuata nyayo za klabu za Simba na Yanga ambazo pia ziliwahi kutinga fainali za mashindano ya Afrika kwa nyakati tofauti.

Ikiwa itafanikiwa kutwaa ubingwa, Serengeti Boys itakuwa sio tu timu ya kwanza ya taifa ya Tanzania kubeba taji la mashindano ya Afrika bali pia itaadndika historia ya kufanya hivyo kwa nchi zinazounda Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).


Fainali bila deni

Hata ikitokea Serengeti Boys imepoteza mchezo huo wa fainali, hakuna sababu ya kuwa na unyonge kwa sababu imeshatimiza lengo la msingi la mashindano hayo ambalo ni kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.

Serengeti Boys ilikata tiketi hiyo ya kucheza Kombe la Dunia 2026 baada tu ya kuingia hatua ya robo fainali ya fainali hizo za Afrika ambazo leo zinafikia tamati nchini Morocco.

Katika Fainali hizo za Kombe la Dunia, Afrika itawakilishwa na timu 10 ambapo mbali na Serengeti Boys, nyingine ni Mali, Cameroon, Algeria, Misri, Morocco, Uganda, Msumbiji, Senegal na Ivory Coast.

Kwa kufuzu Kombe la Dunia la Vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imetimiza ndoto ambayo haikuweza kufikiwa na kaka zao katika Fainali za AFCON U17 mwaka 2017 na 2019.

Mwaka 2017, Serengeti Boys ilishindwa kufuzu Kombe la Dunia baada ya kukwamia katika hatua ya makundi ya Fainali za AFCON ikishika nafasi ya tatu kwenye kundi lake na mwaka 2019 ambapo fainali hizo za Afrika zilifanyika hapa nchini, Serengeti Boys ilishika mkia katika kundi lake.


Noti zanukia

Tayari Serengeti Boys wana uhakika wa kupata fedha kiasi cha Sh500 milioni, kutokana na ahadi ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kama pongezi kwa timu hiyo kufika fainali ya mashindano hayo.

Fedha hizo itapatiwa iwe imeibuka na ushindi au hata ikipoteza mchezo wa kesho.

Ikiwa itapata ushindi kesho, Serengeti Boys pia imepewa ahadi na Rais Samia ya kila mchezaji kupata kiwanja mkoani Morogoro.

Pia timu hiyo itajihakikishia kitita cha Dola 125,000 (Sh329 milioni) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Ifahamike kwamba mshindi wa pili wa mashindano hayo, CAF inampatia kitita cha Dola 90,000 (Sh237 milioni).


Tuzo kemkem

Ushindi wa mchezo wa leo utawaweka Serengeti Boys katika nafasi nzuri ya kuondoka na tuzo nyingi binafsi katika fainali hizo.

Kocha Elieneza Nsanganzelu, ananukia kupata tuzo ya Kocha Bora wa Mashindano huku kipa Haji Ally akiinyemelea tuzo ya Kipa Bora.

Kinara wa kufumania nyavu katika mashindano hayo hadi sasa ni Dismas Athanas wa Tanzania.

Pia kuna uwezekano wa mmojawapo kati ya wachezaji wanne akaibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano ambao nyota hao wanne ni Issa Chole, Razack Mbegelendi, Luqman Mbalasalu na Athanas.


Matumaini juu

Kocha Elieneza amesema kuwa wachezaji wake wamejiandaa vyema na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo. “Tunamshukuru Mungu vijana wote wako salama na wanapumzika vizuri. Watanzania waendelee kuiamini timu yao. Maandalizi yanaendelea vizuri. Tunashukuru serikali imeonyesha kuwa iko nyuma ya timu.

“Senegal ni timu inayopenda kutumia miili. Staili yao ya uchezaji, wanapokuwa na mpira wanataka kufika golini kwa haraka. Hamna fainali ambayo huwa rahisi, utakuwa mchezo mgumu na kwa hatua tuliyofika tutaenda tukichukulia mechi ni ngumu na sisi tuko tayari kucheza na Senegal,” alisema Nsanganzelu.