Kocha Serengeti Boys aanza mikwara
Muktasari:
- Nsanganzelu amesema hana shaka na uwezo wa vijana wake, akieleza kuwa safari yao ya kufika fainali haikuwa kwa bahati bali ni matokeo ya maandalizi mazuri, nidhamu na ujasiri waliouonesha tangu hatua ya makundi.
KOCHA wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu, anaamini kikosi chake kina uwezo wa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, watakapomenyana na Senegal katika fainali itakayopigwa kesho, Jumanne kwenye Uwanja wa Moulay El Hassan, Morocco.
Nsanganzelu amesema hana shaka na uwezo wa vijana wake, akieleza kuwa safari yao ya kufika fainali haikuwa kwa bahati bali ni matokeo ya maandalizi mazuri, nidhamu na ujasiri waliouonesha tangu hatua ya makundi.
Kocha huyo amesema amekuwa akiwajenga wachezaji wake kisaikolojia ili wasije wakabeba presha ya jina la fainali, bali waingie uwanjani kama ilivyo kawaida yao, wakicheza mpira wao wa kawaida bila woga.
“Jambo muhimu kwetu ni kusalia kwenye kile ambacho tumekuwa tukikifanya bila ya kubeba presha ya mchezo, hakuna sababu ya kuhofia chochote, fainali sio kitu cha ajabu, ni mchezo kama michezo mingine, tofauti ni ukubwa wa jina tu lakini uwanjani ni dakika 90 au zaidi,” amesema na kuongeza;
“Naamini ambacho tumekuwa tukiongea na vile ambavyo tumekuwa tukijiandaa basi tunaweza kuweka historia.”
Kocha huyo aliongeza kuwa moja ya mambo yaliyowafikisha hapa ni uimara wa kikosi katika nyakati ngumu, hasa pale walipolazimika kuamua mechi kwa mikwaju ya penalti bila kuyumba kisaikolojia.
Katika hatua ya nusu fainali, Serengeti Boys iliweka rekodi mpya baada ya kuibwaga Misri kwa penalti 4-3 kufuatia sare tasa, matokeo yaliyowapa tiketi ya moja kwa moja kwenda fainali.
Kabla ya hapo, Tanzania ilimaliza kinara wa kundi C ikiwa na pointi sita kufuatia kushinda mechi mbili dhidi ya Msumbiji na Angola kwa mabao 3-0 katika kila mchezo kabla ya kupoteza mechi ya mwisho kwa mabao 2-1 dhidi ya Mali.
Kisha wakaingoa Algeria katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia kutoka sare ya mabao 3-3 kabla ya kukutana na Misri.
Kwa upande wa Senegal, nao wamefika fainali, baada ya kuwang’oa wenyeji, Morocco kwa penalti 7-6 kufuatia sare ya bao 1-1. Simba hao vijana wa Teranga wameendelea kuthibitisha ubora wao kama moja ya mataifa yanayoongoza kwa kuzalisha vipaji vya soka Afrika.
Katika mchezo huo wa fainali, nyota wa Serengeti Boys, Dismas Shida atakuwa akisaka tuzo ya mfungaji bora, kwa sasa ndiye kinara akiwa na mabao matatu huku akifuatiwa na Razaki Mbegelendi ambaye naye ni mchezaji wa timu hiyo ya taifa la Tanzania ambayo tayari inatiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa vijana.
Kwa upande wa Senegal, mchezaji hatari wa kutazamwa ni Souleymane Commissaire Faye na Abdoulaye Toure ambao kila mmoja amefunga mabao mawili.