Selemani Ndikumana freshi Azam

Muktasari:
Ndikumana amejiunga na Azam akitokea timu ya Lierse S.K. ya Ubelgiji akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo.
UONGOZI wa Azam FC umemalizana na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Seleman Ndikumana kwa kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja.
Ndikumana anaingia kwenye kinyang'anyiro cha namba pamoja na nyota wengine Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, Obrey Chirwa wa Zambia pamoja Idd Seleman 'Nado'.
Ndikumana ni mzoefu wa ligi ya Tanzania kwani aliwahi kuichezea Simba msimu wa mwaka 2007 sambamba na Juma Kaseja ambaye kwasasa anakipiga KMC.
Ndikumana amejiunga na Azam akitokea timu ya Lierse S.K. ya Ubelgiji akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', amesema mchezaji amepewa mkataba huo kutokana na mapendekezo ya kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije.
Alisema Ndayiragije alipendekeza jina la mchezaji huyo na baada ya kufanyanae mazungumzo walibaini amemaliza mkataba na timu yake aliyoitumikia na ndipo walifanya naye mawasiliano ili aweze kuja nchini kwaajili ya kumaliana nae.
"Tumempa mkataba wa mwaka mmoja ambao atautumikia akiwa na timu yetu ambayo inatarajia kushiriki mashindano ya ligi ya ndani na kombe la Shirikisho," alisema.