Sawadogo awasha moto mazoezini

Muktasari:
- Aina ya uchezaji wake umewafanya mashabiki kuanza kumfananisha na kiungo wa zamani wa timu hiyo marehemu Patrick Mafisango ambaye alikuwa mtaalamu wa kufanya maamuzi ya haraka uwanjani na kukaba jino kwa jino.
LICHA ya kiungo mkabaji wa Simba, Ismael Sawadogo kuwaonjesha ufundi kidogo mashabiki wa timu hiyo dhidi ya Dodoma Jiji wiki iliyopita, huko mazoezini nako usipime kwani kila mpira unapokuwepo naye anatua wakati huo huo.
Aina ya uchezaji wake umewafanya mashabiki kuanza kumfananisha na kiungo wa zamani wa timu hiyo marehemu Patrick Mafisango ambaye alikuwa mtaalamu wa kufanya maamuzi ya haraka uwanjani na kukaba jino kwa jino.
Mwanaspoti lilifika kwenye mazoezi ya Simba, yaliyofanyika Bunju kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, jamaa aliwakosha mashabiki ambao ghafla wakamkumbuka Mafisango aliyefariki kwa ajali ya gari Mei 17 mwaka 2012.
Katika mazoezi hayo alionekana kupiga pasi zilizonyooka, alihakikisha anakaba kabla mpira haujafika kwa mabeki wake, alikuwa akipanda juu na kushuka kwa haraka kuimarisha ulinzi na wakati mwingine alikuwa anaibia majukumu ya kuichezesha timu, jambo ambalo lilifanya ashangiliwe kwa muda mwingi.
Mashabiki walisikika kuwa jamaa ni balaa ni kama alivyokuwa Mafisango na anahitaji kuongeza mazoezi kidogo ili awe fiti sana basi pale katikati kwenye kikosi cha Simba itakuwa balaa.
Kiwango kinachozidi kuonyeshwa na mchezaji huyo mazoezini kinazidi kuleta ushindani katika eneo la kiungo mkabaji ndani ya kikosi hicho, eneo ambalo pia linachezwa na Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na hata Erasto Nyoni.
Hata katika mazoezi ya wiki hii vita kubwa ya namba imeonekana kuwa kubwa kwani wachezaji wa nafasi hiyo wamekuwa wakipambana mazoezi kila mmoja akitaka kumshawishi kocha kucheza kikosi cha kwanza.
Beki wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah alisema ni kiungo mzuri ila bado ni mapema kuona kama atafanana na Mafisango moja kwa moja.
"Nilitazama ile mechi bado kwa sasa ni ngumu kumfananisha moja kwa moja na Mafisango ingawa kwa muda mchache ameonesha ana kitu mguuni kwake ngoja tumpe muda kidogo.
"Kwa upande wa Mafisango yeye ulikuwa unamuona wakati wa kuzuia, katikati ya uwanja, alikuwa akienda kufunga, anakaba na anatengeneza nafasi huyu Sawadogo kuna baadhi ya vitu anendana naye japo vingine sijaona akivitumia sawa sawa.
" Sawadogo kuna vitu fulani anavyo hasa anapoenda kukaba unaona kabisa ni mtu anakwenda kutafuta mpira, anaweza kwenda mbele na kurudi nyuma kwa haraka zaidi timu inapokuwa ikishambuliwa, tumpe muda kwani uwanja wa Dodoma haukuwa rafiki kwake ngoja tuone katika viwanja vingine tuangalie na uwezo wake zaidi ila ni anaonekana ni bonge la mchezaji," alisema Maftah.