Samia: Ukinizingua tutazinguana

Tuesday April 06 2021
ukinizinguapi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu

By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. “Wewe ni kijana mimi ni mama ukinizingua tutazinguana,” ni kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwenda kwa  mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania  (Tasac),  Kaimu Mkeyenge muda mfupi baada ya kula kiapo cha uaminifu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha watendaji aliowateua wakiwemo makatibu wakuu na manaibu wao.

Katika maelezo yake kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema amemteua Mkeyenge kushika nafasi hiyo ili asafishe madudu yaliyopo kwenye taasisi hiyo.

“Ulikuwa ndani ya Tasac unayajua madudu yaliyopo.  Jambo lililoniudhi zaidi kwa mwaka mmoja mmefanya vikao 23 vya bodi na imetumiwa karibu Sh600 milioni, ukiangalia kilichozungumzwa na tija ya vikao hivyo hakuna.”

“Nataka ukafanye kazi na sio kwenda kupandisha mabega kwa wenzio uliowaacha, kama kuna makundi ukayaondoe, tunataka Tasac izalishe. Nasisitiza kafanye kazi ukinizingua tutazinguana,” amesema.

Rais Samia pia amempa miezi sita mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Erick Hamis kuhakikisha mambo yanakwenda kama inavyostahili.

Advertisement

“Erick ulikuwa Dar es Salaam kwa sababu hizi na zile ukatupwa Mwanza, lakini hukukata tamaa ukafanya kazi nzuri kule na kutokana na mazuri uliyoyafanya Mwanza nimekurudisha hapa ufanye kazi. Najua ndani ya Bandari kuna makundi, usiende kuangalia mtu usoni, nenda kafanye kazi bila kuwa na kundi,” amesema Samia.

Advertisement