Samatta, Bocco wapya waanza kutengenezwa

Muktasari:

  • Wadau mbalimbali wamekuwa wakiwatengeneza vijana kwenye akademi pamoja na kuandaa mashindano madogo madogo kwa ajili ya kupata wale ambao wataonyesha kitu zaidi na kupewa nafasi ya kuendelezwa.

NDOTO ya kutengeneza mastaa wapya kama Mbwana Samatta na John Bocco imeendelea kuonekana baada ya wadau wengi kuwekeza nguvu katika soka la vijana nchini.

Wadau mbalimbali wamekuwa wakiwatengeneza vijana kwenye akademi pamoja na kuandaa mashindano madogo madogo kwa ajili ya kupata wale ambao wataonyesha kitu zaidi na kupewa nafasi ya kuendelezwa.

Kampuni ya Just Fit imekuja na mashindano ya Inter Schools Games ambayo yatashirikisha shule za msingi, sekondari na akademi za michezo zilizopo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukuza vipaji na walengwa ni vijana walio chini ya miaka 12 na 19.

Akizungumzia mashindano hayo, Mkuu wa Idara ya Masoko kutoka kampuni hiyo, Jabir Jabir alisema lengo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika jitihada za kukuza vipaji vya michezo kuanzia rika la chini.

"Tumekuwa tukisapoti  mashindano ya michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa tukaona tuje na aina hii ya mashindano ya michezo mbalimbali ili kuibua vipaji ili baadae tuwe na akina Mbwana Samatta, John Bocco wengine," alisema Jabir.

Upande wa Mkurugenzi wa miradi wa kampuni hiyo, Begum Sykes alisema itahakikisha asilimia 10 itakayopatikana itaenda kuboresha michezo hasa kwenye ukarabati wa miundombinu.

"Mfano kwa sasa tumeshaanza kuboresha uwanja wa mpira wa kikapu pale Ocean Road ambapo moja wa michezo hii itafanyika, tutaendelea kukarabati kadri tutakavyoweza ili vijana waweze kuonyesha vipaji vyao," alisema Sykes.

Mashindano hayo yatakuwa ya siku mbili kuanzia Desemba 9 hadi 10 2023 katika viwanja vya Gymkhana.