Samasoti ni hatari zaidi kwa afya za wachezaji

WACHEZAJI wa soka wametakiwa kuzingatia afya zao kwa kuwaona wataalamu wa afya mara kwa mara ili kuepusha madhara juu yao wawapo uwanjani na kuacha aina hii ya ushangiliaji ambayo inaweza kusababisha kifo.

Hivi karibuni kulitokea sintofahamu baada ya mchezaji wa timu ya KF Egnatia Raphael Dwamena katika ligi nchini Albania kuanguka uwanjani ghafla na kupoteza maisha.


DK RICHARD YOMBA

Daktari wa timu ya Taifa ya Tanzania na Polisi Tanzania Richard Yomba amewataka wachezaji kuwa wakweli hasa linapokuja suala la afya zao kwani kuficha hakuwasaidii lolote.

“Yule mchezaji aliyefariki hivi karibuni timu nyingi zilikuwa zinamkataa kutokana na tatizo la moyo lakini kwa kuwa ni ajira yake kutafuta riziki aling’ang’ania kucheza kwa usalama wa maisha yake hakutakiwa kucheza.”

Alisema kufariki kwa mchezaji uwanjani mara nyingi kunasababishwa na tatizo la moyo ambapo kuna kitu kinaitwa ‘cardic arrest’ hii ndio inawapata mara nyingi sana wachezaji.

“Mchezaji akidondoka ghafla kuna kuwa na vyanzo ikiwamo ugonjwa wa moyo, wanatakiwa wazingatie ‘pre medical checkup’ kwa kuwa mchezo wa soka ni wa kugongana mchezaji unaweza mara kwa mara kufanya chekup ya mwili,” anasema.

Yomba anasema wachezaji wanatakiwa kufahamu wakipoteza maisha atatafutwa mwingine wa kuziba nafasi na maisha yanaendelea hivyo wanatakiwa kuthamini afya zao.

“Unakuta mchezaji anakosa pumzi anasema hali ya hewa kumbe ni tatizo jingine akimuona daktari. Halafu wasifiche matatizo yao kama anaogopa kumwambia daktari wa timu basi amwambie wa nje ili kulinda afya yake.

“Kawaida ya kukamatwa kwa ghafla kwa moyo ni mdundo wa moyo usio wa kawaida unaoitwa fibrillation ya ventricular. Ishara za moyo za haraka na zisizobadilika husababisha vyumba vya chini vya moyo kutetemeka bila maana badala ya kusukuma damu. Hali fulani za moyo zinaweza kukufanya uwezekano wa kuwa na aina hii ya tatizo la mapigo ya moyo.”


AINA ZAKE NA UZUIAJI WAKE

Hizi ni aina za mshtuko wa moyo: Moyo huacha kufanya kazi ghafla, na kusababisha upotezaji wa mtiririko wa damu na mzunguko.

Kukamatwa kwa moyo kwa ghafla: Kukamatwa kwa moyo kunakotokea bila kutarajiwa na kifo cha ghafla cha hutokea. Mshtuko wa moyo husababisha kifo.

Namna ya kuzuia isitokee ni kuhakikisha unadumisha uzito wenye afya, usivute sigara, kula lishe yenye afya, yenye usawa, dhibiti mafadhaiko.

Wakati mwingine dalili nyingine hutokea kabla ya kukamatwa kwa ghafla kwa moyo. Hizi zinaweza kujumuisha:

Usumbufu wa kifua, upungufu wa pumzi, udhaifu, moyo unaodunda kwa kasi, kupepesuka au kudunda uitwao mapigo ya moyo.


DAKTARI JUMA SUFIAN

Daktari wa zamani wa Yanga, Juma Sufian anabainisha kuwa wachezaji wanatakiwa kuwa makini na kuthamini afya zao kwa kufanya vipimo kabla ya msimu na kila mara mchezaji ajipime mwenyewe.

“Mchezaji akiwa ndani ya uwanja damu inakuwa inachemka sana, hivyo akiwa na shida kidogo tu kwenye moyo inaweza kuleta madhara makubwa sana,” anasema.

Sufian anawataadharisha wachezaji kuepuka kufanya mambo ambayo yanaleta uhatarishi kwao akitolea mfano, “Kupiga sarakasi baada ya kufunga bao wakati mchezaji anashangilia sio jambo zuri kiafya maana damu inakuwa kwenye mzunguko mkali, sasa anapobinuka inakuwa sio salama kwake,” anasema.

Sufian anasema, hata timu zinatakiwa kuwa na wataalamu wenye taaluma ya udaktari wa michezo na sio bora daktari tu kwa manufaa ya wachezaji wao.

“Sio kila mtaalam wa tiba ana uwezo huo wa kutibu wachezaji, mfano Jumamosi tulikuwa na kozi ya juu ya ‘sports medicine’ wataalamu kutoka timu mbalimbali za Ligi Kuu walishiriki jambo ambalo ni zuri sana,” alisema.

Kuhusu sarakasi, Yomba anasema inaweza kuchangia mambo mengi yasiyokuwa na afya kwa mchezaji mwenyewe.

“Mchezaji akiruka damu inakuwa kwenye presha kubwa hivyo ligament (kano) na meiniscus (tishu rahisi, laini) akianguka zinaweza kumletea shida ambayo inaweza kuvuja damu na kusababisha madhara makubwa kwake,” alisema.


DAKTARI NASSORO MATUZYA

Aliwahi kuwa daktari wa klabu ya Yanga na anasema mchezaji kupoteza maisha kunasababishwa na vitu vingi, “Moyo kusimama ghafla, head injur (kuumia kichwani), kuziba kwa mfumo wa fahamu hii inatokea mchezaji akianguka anaweza kuziba njia ya hewa na ndio maana mwamuzi ufanya haraka kuwaita madaktari ndani ya kiwanja ikitokea sintofahamu kwa mchezaji,” anasema.

Anasema kingine ambacho kinapelekea hilo ni maradhi binafsi ya wachezaji, kutolewa huduma ndivyo sivyo au kuchelewa kwa huduma navyo visababishi vya kutokea kwa tukio hilo.

Matuzya anasema ikitokea hivyo ndio maana inahitajika mtaalamu mwenye ujuzi ya kuhudumia wachezaji kwa usahihi kutokana na shida iliyompata na sio bora mtaalamu.

“Tatizo kubwa liko katika viongozi wa klabu zetu, mara nyingi unakuta wana daktari wa mifupa na sio wa mchezo na pia changamoto nyingine ni scouting kwenye medical sisi tunajichukulia tu mchezaji kisa anajua mpira kumbe ni pancha akija anasugua benchi na gharama nyingi zimetumika, tunatakiwa kubadilika.”

Anasema mbali na hayo unamkuta mchezaji ana afya ya akili akipangwa tu mechi anaumwa kabisa jambo ambalo mtaalamu wa mchezo anaweza kulibaini haraka kuliko mtaalamu mwingine.

Matuzya anashauri klabu zihakikishe zinawaajiri watu sahihi kama ni mtaalamu wa tiba azingatie kumfuatilia mchezaji kuanzia nyumbani, namna ya kuishi kwake, kula kwake na mambo mengine.

“Inatakiwa kocha asubuhi kabisa anaanza kuongea na daktari ili kufahamu hali za wachezaji wake hapo ataweza kupanga programu zake lakini sisi tunajiendea endea tu madhara yake ni makubwa na ndio mambo yanayofanya kuporomoka kwetu,” anasema Matuzya.


WACHEZAJI WANENA

Aliyekuwa mchezaji wa Dodoma Jiji na sasa Moroka Swallows ya Afrika Kusini, David Uromi anasema akifunga bao kisha akabinuka sarakasi hujisikia mwenye furaha kwa kuwa ni jambo analolifanyia mazoezi mapema.

“Mimi sijawahi kuona madhara yake kwa sababu nimekuwa nikifanya hivyo tangu mdogo na ikitokea nikafunga inategemea na mood nikijisikia kuruka huwa naruka,” alisema.

“Huwa naruka kwa tahadhari sana na ndio maana nawasihi wachezaji wenzangu kama hawana mazoezi wasifanye hivyo maana ikikosea ukaanguka vibaya inaweza ikawa shida.”

Mshambuliaji wa Gwambina iliyokuwa Ligi Kuu, Miraji Salehe aliwahi kukiri baada ya kuruka sarakasi alipata kizunguzungu na kujiona kukosa nguvu kuanzia hapo aliamua kuacha ushangiliaji huo.

“Ni staili nzuri sana ya ushangiliaji lakini kwangu niliamua kuachana nayo baada ya siku hiyo kupata kizunguzungu kikali sana nikaona isije kuniletea shida,” anabainisha.

Simon Msuva mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, anabainisha kuwa anapofunga akipiga sarakasi hujisikia mwenye furaha zaidi lakini kwa kuwa Mwanaspoti imemweleza kuwa inaweza kumletea shida, ataiacha hiyo staili ya kushangilia.

“Nilikuwa najua kuna madhara endapo ukiruka vibaya ukaanguka kumbe kuna zaidi ya hayo basi nitaiacha isijeniletea shida,” anasema.

Oktoba 3, 2021 mshambuliaji wa Yanga kwa sasa, Chrispin Ngushi baada ya kuifungia timu yake ya Mbeya Kwanza bao la kusawazisha katika dakika ya 77 na jingine katika dakika ya 86 aliruka sarakasi iliyomfanya kuanguka chini na kushindwa kuendelea na mchezo.

Baada ya kuanguka katika mchezo huo wachezaji wenzake walidhani anashangilia kumbe mwenzao hali ilibadilika na ndipo madaktari walipomchukua na kumuwahisha hospitalini.

Edmund John wa Geita Gold anasema anapofunga ni vibe linamujia kuruka sarakasi, na hakuwa anafahamu kama inaweza kuwa na madhara kwake.

“Niseme ukweli najirukiaga tu sijui kabisa kama inaweza kuniletea shida sasa umenifungua nitaacha kabisa kufanya hivyo japokuwa ni kastaili ambako nakapenda sana,” anasema.

Mbali na hao wapo wachezaji wengine wengi wanaopenda kushangilia hivyo akiwemo Dickson Ambundo wa Singida Big Stars, Hassan Kabunda wa Namungo, Dickson Kibabage wa Yanga na wengineo.


MAKOCHA HAWAPENDI

Hata hivyo, kocha Ahmed Simba wakati anainoa Copco Veteran aliwahi kuwapiga marufuku wachezaji wa timu hiyo kushangilia kwa staili hiyo ambayo ni hatari kiafya.

Mbali na Simba hata kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson aliwahi kumpiga marufuku mchezaji wake Luis Nani kushangilia kwa kuruka sarakasi kutokana na madhara ambayo angeweza kuyapata.

Wachezaji wengi duniani wamepoteza maisha wakiwa ndani ya mchezo kutokana na sababu mbalimbali akiwemo Papy Faty Raia wa Burundi, Ismail Khalphan Mtanzania alikuwa akikipiga timu ya vijana ya Mbao, Mcameroon Patrick Ekeng, Mkenya Raphael Asud, Herman Tsinga Raia wa Gabon na wengineo.


MWENYE SARAKASI ZAKE

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ kuruka sarakasi baada ya kufunga ilikuwa ndiyo staili yake kubwa mpaka alipotundika daluga.

Katika mazungumzo na Mwanaspoti anasema kabla ya kuanza kusakata kabumbu alikuwa mruka sarakasi na ndio maana aliona aitumie staili hiyo kufurahi kila alipoifungia timu yake mabao.

“Unajua zamani wakati tunacheza hata haya mambo ya kitabibu hayakuwepo kivile tulikuwa tunajichezea tu, kama ningejua kuna shida nikifanya hivyo ningeiacha maana zipo staili nyingi za kushangilia,” anasema na kuongeza kuwa kama ina madhara wachezaji waiache wasipoteze ndoto zao mapema kwa sababu afya ya mchezaji ni muhimu kuliko jambo jingine lolote michezoni.