Saido, Chico wana jambo lao, Nabi aweka wazi mikakati

KOCHA wa Yanga, Nesreddine Nabi ameweka wazi kuwa usajili wa mawinga wengi katika kikosi chake ni kwamba wana kazi spesho msimu huu kwani hawataki kuacha kitu kwenye jambo lao. Kwenye dirisha dogo la usajili Yanga wameongeza mawinga watatu na sasa wanao saba. Mawinga waliokuwa katika kikosi cha Yanga, Lucapel Moloko, Saido Ntibazonkiza, Deus Kaseke, Dickson Ambundo, Nkane, Chico Ushindi na Yacouba Sogne ambaye ni majeruhi.
Nabi alisema aina ya uchezaji ya kila mchezaji ni tofauti,Moloko ni mzuri kwenye kukimbia na kuwalazimisha mabeki hata muda mwingine kuchezewa faulo, anaweza kutengeneza nafasi za kufunga na muda mwingine hufunga mwenyewe ndio maana mpaka sasa kwenye ligi amefunga matatu.
“Ntibazonkiza anaweza kukokota mpira kutokea pembeni na akapiga pasi ya bao au kufunga mwenyewe ndio maana mpaka sasa amefunga manne, anaweza kupiga mipira iliyokufa kama kosa na faulo ambazo zinazaa mabao, muda mwingine hucheza kutokea katikati kama kiungo,” alisema Nabi na kuongeza mawinga wake wote hawafanani.
Alisema ameifuatilia Yanga na kubaini miongoni mwa eneo ambalo ni bora hata miaka ya nyuma mawinga ndio maana hata kwake ameboresha eneo hilo na limekuwa linalipa.
“Inaweza kutokea siku moja nisiwepo hapa au hata wakati mwingine nimefikiria kuwa na mawinga bora katika siku za mbele kama Nkane na Ambundo kutokana na umri wao mdogo,” alisema Nabi na kuongeza;
“Huyu Nkane nilimuona akiwa na Biashara United, amesajiliwa na Yanga nimempa nafasi kwenye Mapinduzi amefanya vizuri ikiwemo kufunga bao hiyo ni mapema itakuaje akiwa ndani ya kikosi kwa muda mrefu na akazoea, maana yake atakuwa bora zaidi, Ambundo nilikuwa nae kwenye mazoezi baada ya kupata majeraha nyakati tofauti alikuwa anaonyesha kiwango bora na kutimiza majukumu yake vile ambavyo nahitaji, nilimpa nafasi kwenye Mapinduzi amefanya vizuri.
“Katika kuonyesha anatamani kucheza zaidi hakuridhika na ubora wake bali alifanya zaidi mazoezini, kwenye mechi ngumu ya ligi dhidi ya Polisi Tanzania na akafanya vizuri zaidi ya vile mazoezini na akafunga bao muhimu,” aliongeza.
USHINDI HUYU HAPA
Nabi alisema Ushindi ni miongoni mwa mawinga wazoefu waliocheza mechi kubwa na zenye ushindani kikosi cha TP Mazembe.
“Ushindi aina yake ya uchezaji ni tofauti kabisa na wale wengine waliokuwepo katika kikosi na akizoea mazingira ataofa vitu,anatengeneza nafasi za kufunga, kufunga mwenyewe na kuhusika katika mabao.Wala sina wasi wasi tunamechi nyingi msimu huu kwenye kombe la Shirikisho (ASFC) na Ligi Kuu Bara,” alisema.