Saido aondoka, Simba mzigoni

Muktasari:

  • Kikosi cha Simba kinarejea mazoezini leo kufuatia wachezaji wa timu hiyo kupewa mapumziko ya siku tatu baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania uliopangwa kuchezwa leo kupigwa kalenda hadi Juni 6, lakini mastaa hao watatu hawatacheza mchezo wowote msimu huu.

KIUNGO wa Simba Saido Ntibazonkiza ameungana na Clatous Chama na Inonga Baka kumaliza msimu mapema, baada ya juzi kuomba kwa uongozi wa timu ruhusa ili akapumzike, timu ikirejea mzigoni.

Kikosi cha Simba kinarejea mazoezini leo kufuatia wachezaji wa timu hiyo kupewa mapumziko ya siku tatu baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania uliopangwa kuchezwa leo kupigwa kalenda hadi Juni 6, lakini mastaa hao watatu hawatacheza mchezo wowote msimu huu.

Chama hatacheza baada ya kufungiwa michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara kutokana na utovu wa nidhamu, lakini awali Inonga aliomba ruhusu akapumzike, huku juzi Saido naye akipeleka ombi ambalo linadaiwa kuwa lilikubaliwa.
Simba ilikuwa inaikaribisha Polisi Tanzania leo ila kitendo cha

Yanga kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kimeifanya Bodi ya Ligi (TPLB), kusogeza mbele michezo yote ya mzunguko wa 29, 30 hivyo itachezwa Juni 6 na 9.

Awali ratiba ilikuwa inaonyesha Ligi itafikia tamati Mei 28 ila kutokana na siku hiyo ndio fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, TPLB imeona ni vyema kusogeza mbele ili kuepuka upangaji wa matokeo hasa timu zilizoko mkiani.

Kutokana na hali hiyo Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' alisema wakati wanarejea mazoezini leo wataweka mikakati mipya ya timu hiyo kutokana na kutocheza mchezo wowote wa ushindani hadi hapo Juni 6.

"Tulikuwa tayari kwa mchezo wa leo na ujao wa kukamilisha ratiba lakini baada ya kupokea barua ya TPLB ya kuahirisha michezo yote ilibidi kubadilisha programu hivyo leo tunakutana kuangalia cha kufanya," alisema.

Aidha Robertinho aliongeza licha ya utayari wa wachezaji wa timu hiyo ila mabadiliko hayo hayawezi kuathiri kwani atakaa kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi kutafuta njia mbadala itakayowaweka kwenye ushindani.

"Tunahitaji kupata angalau michezo miwili ya kirafiki ambayo tutaitumia kuwaweka wachezaji katika ushindani kabla ya kurejea katika mechi za mwisho ingawa hilo litategemea na makubaliano yetu ya pande zote mbili."

Mbali na mchezo na Polisi Tanzania ila Simba itaendelea kusalia jijini Dar es Salaam kwani hata mechi yake ya mwisho ya kumalizia msimu dhidi ya Coastal Union itapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Hata hivyo, inafahamika kuwa Simba wanakwenda tu kumalizia msimu, wakiwa hawana chochote wanachoweza kuvuna, kwani tayari Yanga wameshatwaa ubingwa nao wana uhakika wa kumaliza kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.