Sababu yakipigo cha Serengeti Girls
Muktasari:
- Serengeti Girls ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, na kuifanya Uganda ikitwaa ubingwa huo.
NAHODHA wa Serengeti Girls, Elizabeth John amesema hawajui nini hasa kilitokea hadi kushindwa kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa fainali ya Michuano ya CECAFA U-17 dhidi ya Uganda akikiri walicheza chini ya kiwango.
Serengeti Girls ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, na kuifanya Uganda ikitwaa ubingwa huo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Elizabeth alisema walionekana kuwa na hofu jambo ambalo lilichangia kushindwa kucheza kwa kujiamini kama walivyofanya katika mechi nyingine za hatua ya makundi na nusu fainali.
"Kwa kweli hatukucheza vizuri kabisa na hata mimi sijui nini kilitokea labda ilikuwa ni hofu kwa sababu tangu mechi ilipoanza hatukuwa kwenye kiwango chetu cha kawaida. Uganda walikuwa bora zaidi yetu," alisema Elizabeth.
Nahodha huyo alisema licha ya kupoteza kombe likiwa nyumbani, wamejifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia katika mashindano yajayo na hasa wanapokutana na timu zenye ushindani mkubwa.
"Ni somo kubwa kwetu tumegundua kuwa tunahitaji kucheza mechi nyingi zaidi za ushindani ili kuzoea presha ya michezo mikubwa kama hii haya ni mambo ambayo yatatusaidia kukua zaidi kama timu," alisema.
Licha ya kupoteza fainali hiyo, Serengeti Girls ilionyesha kiwango kizuri katika mashindano hayo baada ya kumaliza hatua ya makundi bila kupoteza mechi yoyote. Timu hiyo ilianza kwa kuifunga Somalia mabao 4-0, ikaichapa Sudan Kusini mabao 10-0 kabla ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Kenya.
Katika hatua ya nusu fainali, Serengeti Girls iliiondosha Sudan Kusini kwa mabao 4-0 na kutinga fainali ikiwa moja ya timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo.