Sababu ya Tanzanite kufungwa

BAADA ya kutolewa katika mbio za kufuzu Kombe la Dunia kwa timu za Taifa za wanawake chini ya miaka 20, kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Tanzanite Queen’, Bakari Shime amesema sababu kubwa iliyochangia kutolewa ni uwanja walioutumia kwa mechi ya marudiano nchini Nigeria.

Tanzania ilitolewa juzi kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Moshood Abiola.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza baada ya mchezo kumalizika, Shime alisema uwanja uliwafanya washindwe kucheza soka la siku zote badala yake watumie njia ya kupiga mipira mirefu mbele. “Uwanja haukuwa rafiki sana kwetu. Kwa hiyo ilibidi tubadili aina ya kucheza soka la chini na kutumia mipira mirefu kupeleka mashambulizi,” alisema.

“Tulipambana hadi tunakwenda mapumziko tulikuwa 1-1, lakini kwenye kipindi cha pili wenzetu walipata kona na kuitumia vizuri wakapata bao. Tulipambana kuweza kusawazisha lakini haikuwa hivyo.”

Shime aliongeza kuwa: “Tumetoka kwenye mashindano lakini bado kuna kitu kipo kwenye timu yetu na kuna mashindano mengine ambayo naamini tutafanya vizuri.”