Sababu mbili Yanga kucheza Mwanza

Muktasari:

Tangu mwaka 2016, Yanga imecheza mechi 16 za kimataifa kwenye uwanja huo, imeibuka na ushindi mara saba, kutoka sare saba na kupoteza michezo miwili.

Dar es Salaam. Hofu ya matokeo yasiyoridhisha katika mechi za kimataifa na presha ya mashabiki zinaonekana kama sababu mbili zilizochangia Yanga kuhamishia mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Wakati Yanga ikiwa haina rekodi ya kuvutia inapocheza mechi za kimataifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wadau mbalimbali wametetea uamuzi wa kupeleka ugenini mchezo wa kwanza wa hatua ya mchujo dhidi ya timu hiyo.

Tofauti na ilivyozoeleka kwa Yanga kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mechi za kimataifa, safari hii itacheza CCM Kirumba - uamuzi ambao umechagizwa na mapendekezo ya benchi la ufundi.

“Sababu kubwa iliyofanya tupeleke mechi Mwanza ni uwanja kwa sababu tutakuwa tumeshauzoea. Hatuwezi kucheza mechi Mwanza na Mbao, Oktoba 22 halafu upumzike uanze safari ya kurudi Dar es Salaam upumzike siku moja halafu ufanye mazoezi na kesho yake ucheze na Pyramids, utawachosha wachezaji,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela jana.

Wakati Yanga ikitaja sababu za kiufundi kama chanzo cha kuhamishia mchezo huo Mwanza, rekodi ya kutofanya vyema katika mechi za kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa inaonekana kama sababu iliyowapa hofu ya kucheza dhidi ya Pyramids jijini hapa.

Yanga imepata ushindi mara moja katika mechi tano za mwisho za kimataifa ilizocheza Uwanja wa Taifa, ikitoka sare mara tatu na kupoteza moja.

Timu hiyo imefunga mabao sita na wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara sita na wapinzani wao tofauti.

Tangu mwaka 2016, Yanga imecheza mechi 16 za kimataifa kwenye uwanja huo, imeibuka na ushindi mara saba, kutoka sare saba na kupoteza michezo miwili.

Kwa namna moja, rekodi hiyo inaonekana kama moja ya sababu zinazoweza kuwaathiri wachezaji wao kisaikolojia na kuwafanya wacheze kwa hofu ambayo inaweza kuwanufaisha wageni.

Lakini pia presha ya mashabiki ambao wamekuwa hawaridhishwa na kiwango cha timu yao, inaonekana kama sababu nyingine ya timu hiyo kutimkia Mwanza ili kuwaweka wachezaji wake kwenye hali ya utulivu katika maandalizi ya kujiandaa na mchezo huo.

Hata hivyo, licha ya Yanga kuhamia Uwanja wa CCM Kirumba, bado hata huko nako imekuwa haina rekodi ya kujivunia pindi inapocheza mechi za kimataifa.

Katika michezo mitatu ya miaka ya karibuni iliyocheza kwenye uwanja huo ilitoka sare zote dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mabao 3-3 katika pambano lililopigwa Mei 26, 2001 na Mei 6, 2007 ilipata suluhu dhidi ya El Merreikh ya Sudan, huku Aprili 21, mwaka huo ikitoka suluhu na Esperance ya Tunisia.

Lakini wakati rekodi zikionyesha kuwa Yanga haijawahi kupata ushindi kwenye mechi za kimataifa ilizocheza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wadau mbalimbali wa soka wametetea uamuzi huo ingawa wameishauri ijiandae vilivyo kwa ajili ya mechi hizo.

“Suala la kupeleka mechi Mwanza au kutopeleka ni la uongozi mzima wa Yanga, nafikiri wamefanya utafiti na wakashauriana na mwalimu wameona wakicheza kule wanaweza wakapata matokeo,” alisema Charles Mkwasa, kocha wa zamani wa timu hiyo.

“Maandalizi ya kupata matokeo mazuri inategemea mtakavyokuwa mmejipanga na kuweza kuona nini mtafanya siku hiyo.

“Uwanja ndio miundombinu ya kwanza kuipa timu ushindi, kikubwa inategemea namna mtakavyoutumia. CCM Kirumba sio uwanja wa kiwango cha chini, ile sehemu ya kuchezea inaendana na ile ya Uwanja wa Taifa ambao kidogo nyasi zake ziko vizuri zaidi kuliko Kirumba.

“Pia mpira ni kujipanga, ukijipanga vizuri utaweza kucheza popote na ukapata matokeo mazuri ingawa uwanja huohuo pia unaweza ukasababisha usicheze vizuri.”

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema moja ya sababu ambayo amewaelewa Yanga lengo lao la kupeleka mechi CCM Kirumba ni kutaka kupata mashabiki wengi.

“Ukiangalia hiyo ya kutaka kupata mashabiki wengi watakaojaza uwanja siku hiyo ndio sababu ya msingi zaidi ambayo naiunga mkono mechi hiyo kuchezwa Mwanza,” alisema Mayay, ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo.

“Mwanza hawajapelekewa siku nyingi mechi za kimataifa kitendo cha kupeleka mechi hiyo kule watapata hamasa kutoka kwa mashabiki na watajaza uwanja.”