Ronaldo kupewa uwanja wa mpira Ureno

Muktasari:

Klabu ya soka ya Sporting Lisbon inafikiria kulibadili jina la uwanja wao wa Estadio Jose Alvalade ili uitwe jina la staa wao huyo wa zamani, Cristiano Ronaldo.

LISBON, URENO. Mshambuliaji Cristiano Ronaldo tayari ana uwanja wa ndege na nyota zilivyopachikwa jina lake ukiachana na dawa ya kunyolea, sanamu na mavazi ya ndani, ambayo yamekuwa yakifahamika kwa jina la staa huyo wa Juventus.
Lakini, sasa CR7 anaweza kupata kitu kingine kipya cha uwanja wa soka kupachikwa jina lake kama heshima ya kile alichokifanya kwenye soka.
Klabu ya soka ya Sporting Lisbon inafikiria kulibadili jina la uwanja wao wa Estadio Jose Alvalade ili uitwe jina la staa wao huyo wa zamani, Cristiano Ronaldo.
Ronaldo alianzia maisha yake ya soka kwenye klabu hiyo kabla ya kwenda kutamba huko Manchester United kisha Real Madrid na sasa Juventus. Kwenye kikosi cha Sporting alianzia kwenye timu ya watoto na kisha kuja kuichezea kwenye msimu mmoja kwenye Primeira Liga kabla ya kunaswa na Man United mwaka 2003.
Rais wa klabu hiyo, Federico Varandas alisema kwamba suala la kubadili jina la uwanja huo lipo kwenye mchakato.
"Ni mpango tunaoufanyia kazi na hakika ni kitu tunachojivunia. "Cristiano yupo na siku zote atabaki kuwapo, akiwa mmoja wa nembo imara kabisa katika historia ya klabu hii," alisema.
"Tunajivunia kuhusika na Cristiano Ronaldo na jina hilo la mchezaji bora kabisa duniani lilitokea hapa Sporting."
Uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 50,000 wanaoketi ulijengwa 1956 na Jose Alvalade, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Sporting Lisbon alikuwa mjumbe wa kwanza wa timu Julai 1906.