Ronaldo atimiza ndoto ya utotoni
Muktasari:
Vyombo vya habari vya kimataifa vilimpanga Ronaldo alikuwa katika ubora wa juu, kuanzia Beijing hadi Los Angeles, kutoka Johannesburg hadi Reykjavik, waandishi wa habari waliotakiwa kupiga kura na jarida la soka la Ufaransa ambalo limekuwa likitoa tuzo hizo tangu mwaka 1956, waandishi hao walimsifia Ronaldo kuwa na kipaji cha kipekee.
TOLEO lililopita Mwandishi Luca Caioli alizungumzia bao la Ronaldo alilofunga kama staa wa mpira wa kikapu anavyodanki, pia alilizungumzia bao la Barca lililofungwa na Messi baada ya pasi 27 zilizopigwa kwa sekunde 75 kabla ya Messi kuujaza mpira wavuni. Sasa endelea.
Kila mchezaji alikuwa na nafasi yake katika bao hilo, pasi 27 za maana katika sekunde 75, mpango mzuri kiuchezaji ambao uliishia kwa Messi aliyeupiga mpira mfupi kwa kasi na kumshinda kipa wa Roma, Wojciech Szczesny.
“Hongera Messi, hata watakaoumizwa wanakukubali,’’ liliandika gazeti la michezo la Marca baada ya Messi kuonyesha soka la juu akiwa na Barca na kuiwezesha timu hiyo kufuzu 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu huo.
Inafahamika kwa wengi kwamba ni ndoto ya Ronaldo tangu akiwa mdogo, na ndoto hiyo ilikuwa kweli mwaka 2008, tuzo yake ya kwanza ya Ballon d’Or. Ni baada ya kuvuna pointi 446 kati ya pointi 480.
Alimbwaga Messi kwa ushindi mkubwa, staa huyo wa Barca alipata pointi 281 ingawa alikuwa na msimu mzuri lakini timu yake ya Barca haikutwaa taji lolote la maana.
Vyombo vya habari vya kimataifa vilimpanga Ronaldo alikuwa katika ubora wa juu, kuanzia Beijing hadi Los Angeles, kutoka Johannesburg hadi Reykjavik, waandishi wa habari waliotakiwa kupiga kura na jarida la soka la Ufaransa ambalo limekuwa likitoa tuzo hizo tangu mwaka 1956, waandishi hao walimsifia Ronaldo kuwa na kipaji cha kipekee.
Na ingawa hakung’ara Ulaya na sanaa zilizotawala uwezekano wa kuhamia Real Madrid, uvumi kuhusu maisha yake binafsi na tabia nyingine za ajabu ajabu na mara nyingine utata uwanjani, bado ni Ronaldo ndiye aliyetangazwa kuwa mshindi.
Katika yote hayo kilichoangaliwa ni kiwango chake cha uhakika uwanjani, kipaji cha aina yake, mabao ambayo yalimpa tuzo ya kiatu cha dhahabu katika Ligi Kuu England na taji la Ligi ya Mabingwa alilotwaa akiwa na jezi ya Man United.
Akiwa ndio kwanza ana miaka 23, Ronaldo akaweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tano mwenye umri mdogo kunyakua tuzo hiyo. Pia, akawa mchezaji wa nne wa Man United na wa kwanza katika Ligi Kuu England tangu Michael Owen atwae tuzo hiyo mwaka 2001.
Ronaldo anafahamu kwamba mwaka 2008 ulikuwa mwaka wake licha ya kutofanya vizuri akiwa na Timu ya Taifa ya Ureno katika fainali za Euro 2008, wakati ambao hapana shaka kwamba alicheza huku akiwa na tatizo la enka.
Alijitetea kwenye gazeti la Italia la Gazzetta dello Sport siku chache kabla ya hafla ya utoaji wa tuzo: “Nafikiri nimefanya mengi ya kutosha kubeba tuzo hii kuliku mtu mwingine yeyote.”
Desemba 7, Ronaldo aliyekuwa mwingi wa furaha alielekea Paris akiwa na familia yake yote kwa ajili ya kupokea tuzo hiyo, alivaa suti ya rangi nyeusi na tai pamoja na shati lenye rangi ya kijivu na nyeupe huku nywele zake akiwa amezichana kwa staili ya kuzielekeza kwa nyuma.
“Kama ambavyo kila mtu anafahamu kwamba kushinda Ballon d’Or ni kitu ambacho nimekuwa nikikiota tangu nikiwa mdogo na ndio maana hili ni tukio lenye kuvutia na kupendeza kwangu, napenda kuchukua fursa hii kuitoa tuzo hii kwa familia yangu ambayo iko hapa pamoja name,’’ alisema Ronaldo na kuwageukia wapendwa wake.
“Naitoa kama heshima kwa mama yangu, baba yangu, dada zangu Elma na Katia, kaka yangu Hugo na marafiki yangu wa karibu Rodrigo na Ze pamoja na wakala wangu, Jorge Mendes, ni jambo gumu kuna wengi wa kuwataja lakini ni kwamba nimefurahi sana.”
Itaendelea
Jumanne ijayo…