Ronaldo akana madai ya kumtukana Messi

Muktasari:
Mwandishi mahiri wa michezo wa Hispania, Guillem Balague ameandika katika kitabu chake kuwa Ronaldo amekuwa akimtukana Messi kwa majina tofauti na habari hiyo imezua zogo kubwa nchini Hispania.
JOTO la upinzani kati ya staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na nyota wa Barcelona, Lionel Messi sasa linaingia katika uhasama baada ya kudaiwa kuwa Ronaldo amekuwa akimtukana Messi pindi akiwa na wachezaji wenzake wa Real Madrid.
Mwandishi mahiri wa michezo wa Hispania, Guillem Balague ameandika katika kitabu chake kuwa Ronaldo amekuwa akimtukana Messi kwa majina tofauti na habari hiyo imezua zogo kubwa nchini Hispania.
Hata hivyo, Ronaldo amesisitiza kupitia mtandao wake kwamba habari hizo siyo za kweli na hajawahi kumtukana Messi, huku akitishia kuchukua hatua za kisheria.
“Habari zinazunguka zikinishutumu kwamba nimekuwa nikitoa maneno machafu dhidi ya Lionel Messi. Habari hizi ni za uongo na nimemwambia mwanasheria wangu achukue hatua kwa wote wanaohusika,” aliandika Ronaldo katika mtandao wake.
“Nina heshima kubwa kwa wanasoka wenzangu wote wa kulipwa na Messi hana tofauti na nao,” aliongeza Ronaldo mwenye umri wa miaka 29 kwa sasa.
Katika kitabu cha Balague, ameelezea uhusiano baina ya wachezaji hao wawili akidai kwamba hawana urafiki wowote lakini wamekuwa wapole mbele ya jamii kwa ajili ya kuvifurahisha vyombo vya habari.
Mwandishi huyo mkongwe amedai kwamba wachezaji kadhaa wa Real Madrid wamempa taarifa kwamba siyo tu Ronaldo amekuwa akimtukana Messi peke yake, bali mtu yeyote anayemuona anaongea na Messi.
“‘Ronaldo, labda kwa kuonyesha dalili za kutopevuka kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa sasa, anadhani kuna umuhimu wa kuweka sura ya kishujaa mbele ya wachezaji wenzake na kutomhofia Messi kwa ajili ya kupambana naye,” anaandika Balague.
“Lakini yote hayo ni uongo na ndio maana, kwa mujibu wa baadhi ya wachezaji wa Real Madrid, Ronaldo amekuwa akimtukana Messi kwa matusi mbalimbali na akimuona mtu yeyote klabuni kwao anaongea na Messi huwa anaishia kumtukana.”
Kwa sasa Ronaldo yupo katika kikosi cha Ureno akijiandaa na mechi za kufuzu kwa Euro 2016 ambapo kesho wanakipiga dhidi ya Armenia.
Messi jana alikuwa anatarajiwa kuiongoza Argentina dhidi ya Croatia katika Uwanja wa West Ham, Rush Green.
Wawili hao wanatazamiwa kukumbana uso kwa uso Jumanne ya wiki ijayo katika pambano la kirafiki baina ya nchi zao litakalopigwa katika Dimba la Old Trafford.