Rodrygo : Kinda wa Brazil aliyeanza kutesa Santiago Bernabeu

Muktasari:

Julai 21, 2017 alisaini mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa baada ya kukubali dili la miaka mitano.

MADRID, HISPANIA . KINDA wa Kibrazil wa Real Madrid, Rodrygo katikati ya wiki hii aliwashtua mashabiki wa soka kwa kupiga Hat trick katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Galatasaray. Mashabiki wamekuwa wakijiuliza, Rodryigo ni nani hasa?

Jina lake kamili ni Rodryigo Silva de Goes na alizaliwa katika eneo la Osasco nchini kwao Brazil mnamo Januari 9, 2001. Ni mmoja kati ya mastaa wachache wa soka wanaotamba barani Ulaya ambao wamezaliwa baada ya mwaka 2000 kuingia.

Alianza kucheza soka katika timu ya vijana ya klabu maarufu ya Santos ambayo inajulikana kwa kuwatoa mastaa wakubwa wa Brazil kama Pele na Neymar.

Awali alianza kuichezea timu hiyo katika mchezo wa soka la sakafuni maarufu kama futsal ilikuwa mnamo mwaka 2011.

Machi 2017 huku wachezaji wa kikosi cha kwanza wakiwa wameitwa katika pambano la michuano ya klabu bingwa Amerika Kusini maarufu kama Copa Libertadores dhidi ya Sporting Cristal ya Peru, Rodrygo aliitwa na kocha wa kikosi cha kwanza Dorival Júnior kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Julai 21, 2017 alisaini mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa baada ya kukubali dili la miaka mitano.

Novemba Mosi alipelekwa katika kikosi cha kwanza kilichokuwa chini ya kocha wa muda, Elano ambaye ni staa wa zamani wa Manchester City.

Alicheza pambano lake la kwanza katika kikosi cha kwanza Novemba 4, 2017 akiingia dakika za mwishokuchukua nafasi ya Bruno Henrique katika pambano dhidi ya Atlético Mineiro waliloshinda mabao 3-1.

Januari 25 akafunga bao lake la kwanza la timu ya wakubwa katika ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya Ponte Preta.

Alicheza mechi yake ya kwanza ya michuano ya Copa Libertadores mnamo Machi Mosi 2018, akichukua nafasi ya Eduardo Sasha katika kichapo cha mabao 2–0 walichopokea ugenini kwa Real Garcilaso.

Siku 15 baadae alifunga bao lake la kwanza la michuano hiyo akifanya juhudi binafsi katika ushindi wa mabao 3–1 dhidi ya Nacional Uwanja wa Pacaembu.

Akafunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ya Brazil mnamo April 14, 2018 katika pambano dhidi ya Ceara ambalo walishinda mabao 2-0. Juni 3 akafunga Hat Trick katika ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Vitoria huku akipika bao jingine lililofungwa na Gabriel.

Julai 26, 2018, Rodrygo alibadilisha namba yake ya jezi kutoka namba 43 mpaka namba 9 ambayo tayari alishaivaa katika pambano dhidi ya Libertadores. Msimu wa mwaka 2019 alibadili namba tena kwenda 11 ambayo awali ilikuwa inavaliwa na Neymar.

Atinga Madrid, aweka rekodi

Juni 15, 2018 Real Madrid ilitangaza kufikia makubaliano na Santos kwa ajili ya uhamisho wa Rodrygo huku mchezaji huyo akitazamiwa kujiunga na Madrid Juni 2019 kwa mkataba wa miaka mitano.

Uvumi ulidai Santos wangepewa kiasi cha Euro 40 milioni kutokana na kummiliki mchezaji huyo kwa asilimia 80 huku hisa zilizobaki zikimilikiwa na mawakala wake.

Septemba 25, 2019 alicheza mechi yake ya kwanza ya timu ya wakubwa katika jezi ya Madrid katika pambano dhidi ya Osasuna ambapo hapo hapo alifunga bao lake la kwanza.

Katikati ya wiki hii alipiga Hat trick dhidi ya galatasaray katika pambano la Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Katika pambano hilo Madrid walishinda mabao 6-0 na kwa kufunga hat trick hiyo alikuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa karne ya 21 kufunga katika michuano hiyo mikubwa zaidi barani Ulaya. Alifunga bao hilo akiwa na miaka 18 na siku 301.

Kwa kupiga Hat trick hiyo pia, Rodrygo alikuwa mchezaji wa pili mdogo wa Real Madrid kufunga Hat trick katika Ligi ya mabingwa wa Ulaya huku wa kwanza akiendelea kuwa Raul Gonzalez ambaye Oktoba 1995 alipiga Hat trick dhidi ya Ferencvarosi akiwa na miaka 18 na siku 113.

Atarajiwa kuitwa Brazil

Mpaka sasa Rodrygo hajaitwa katika kikosi cha wakubwa cha Brazil lakini anaweza kuitwa muda wowote kuanzia sasa kutokana na kiwango chake akiwa na Madrid. Aliitwa katika kikosi cha Under 17 cha Brazil katika michuano maarufu ya Montaigu mnamo Machi 30, 2017.

Alicheza mechi yake ya kwanza katika pambano dhidi ya Denmark walilofungwa 2-1 lakini akafunga mabao mawili dhidi ya Cameroon na Marekani.

Machi 7, 2018, Rodrygo na mchezaji mwenzake wa Santos, Yuri Alberto waliitwa katika kikosi cha Brazil chini ya umri wa miaka 20.

Hata hivyo, siku sita baadae wote wawili waliondolewa katika kikosi hicho kufuatia maombi ya Rais wa klabu yao.

Kwa mujibu wa kumbukumbu baba yake Rodrygo, Eric, ni mwanasoka wa zamani. Alikuwa akicheza kama mlinzi wa kulia lakini hakuwa kucheza katika Ligi yoyote kubwa zaidi ya kucheza katika Ligi daraja la kwanza nchini Italia maarufu kama Série B.