Robertinho kaondoka, Mgunda aachiwa kazi

KIKOSI cha Simba kinarejea kwenye matizi leo lakini Kocha Mbrazili, Roberto Oliveira Robertinho jana usiku aliondoka nchini kwenda kwao. Hiyo  ni muda mfupi baada ya kukiongoza kikosi chake kushinda bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Wachezaji baada ya kutua Dar es Salaam jana walipewa mapumziko ya siku moja na leo jioni  wataanza mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Coastal Union.
Sababu iliyomfanya Robertinho kuondoka nchini ni hati yake ya kusafiria kumalizika muda wake na hakuna hata karatasi moja iliyo wazi na  hivi karibuni atatakiwa kuanza kusafiri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Robertinho baada ya kuwasili Dar alikwenda hotelini  Mbezi Beach kufanya maandalizi ya safari kwenda kwao Brazil na aliithibitishia Mwanaspoti kwamba anakwenda fasta anageuka.
Robertinho atarejea nchini Januari 31, kwa maana hiyo ataukosa mchezo wa ASFC dhidi ya Coastal na kikosi cha Simba kitakuwa chini ya kocha, Juma Mgunda.
Robertinho ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Zoezi la kupata Pasipoti mpya kwetu Brazil ni zoezi la muda mfupi, kwahiyo nitarudi hapa Januari 31, kwa ajili ya kuendelea na ratiba nyingine za timu.”
“Mechi ya FA sitakuwepo timu itakuwa chini ya Mgunda na wasaidizi wengine naamini atafanya vizuri kwani mpango wote wa mazoezi pamoja na mechi itakavyochezwa nimeshamuachia hapa naamini kila kitu kitakuwa sawa.
“Suala hili la kuondoka kwa muda wa wiki moja halitaathiri jambo lolote ndani ya timu kwani kila kitu kuhusu masuala ya kiufundi yote yapo vizuri na wachezaji waliokosekana kwenye mechi iliyopita wengine watakuwa wanerejea,” aliongeza Kocha huyo anayeamini kwenye soka la kushambulia.
Anasema kwamba alikuja nchini mara moja kwaajili ya kumalizana na Simba na kuweka mazingira mazuri ya kuanza kazi na sasa anaamini kuwa akirudi ndio mambo yatanoga. Kocha huyo anasema kwamba mastaa wote wa Simba wako kwenye hali nzuri na wanazungumza lugha moja mazoezini ndio maana anaamini kuwa ndani ya muda mfupi ijayo mambo yatakaa sawa na timu itacheza soka la hali ya juu na lengo lake na Mgunda ikiwa ni kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika na inawezekana kutokana na malengo ya klabu.