RESPECT

Sunday May 09 2021
RESPECT PIC
By Waandishi Wetu

HII ni mechi au bonanza? Ndilo swali lililoulizwa na wadau wa soka, baada ya pambano la watani wa jadi la Simba na Yanga kuahirishwa saa mbili kabla ya kuchezwa jana jioni.

Simba na Yanga zilikuwa zivaane saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, lakini ghafla ikatangazwa kupelekwa mbele hadi saa 1 usiku kwa madai ni agizo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuwatibua mashabiki wa soka, hususan wa Yanga ambao waliamua kusimamia kanuni za kuahirishwa kwa muda wa mchezo na kuivua nguo TFF na Bodi ya Ligi wanaosimamia kanuni hizo.

kuahirishwa pic

Bila ya gharama ya maandalizi ya pambano hilo na viingilio vilivyolipwa na mashabiki waliojihimu mapema uwanjani hapo, mechi ilitangazwa kuahirishwa saa 12:15 jioni baada ya Yanga kuondoka mapema uwanjani wakisimamia kwenye kanuni za soka za kuahirishwa kwa muda wa mchezo.

Mapema baada ya tangazo la TFF kuahirishwa kwa mchezo huo, Yanga ilitoa tangazo la kutokubali mechi kuahirishwa kienyeji kinyume na kanuni ya soka inayoelekeza taarifa ya kuahirishwa inapaswa kutolewa saa 24 kabla ya muda wa mchezo husika.

Yanga ilisisitiza haiafiki kusogezwa mbele kwa mchezo huo kwani ni ukiukwaji wa kanuni namba 15 (10) ya Ligi Kuu inayohusu utaratibu wa mchezo ambayo inasema “Mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali.”

Advertisement

Kuahirishwa kwa pambano hilo lililokuwa la 106 kuliwafanya mashabiki kucharuka kudai lazima warudishiwe fedha za viingilio, huku wakilitupia lawama Shirikisho la Soka (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kwa madai ya kuleta siasa kwenye soka na kukiuka kanuni zinazowaongoza za kuahirisha mechi, huku askari polisi wakilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki waliogoma kuondoka uwanjani baada ya mchezo.

HALI ILIVYOANZA

Tangazo la mechi kuahirishwa lilitolewa na TFF saa 8 mchana wakati timu zikiwa kwenye maandalizi ya kwenda uwanjani, huku ikielezwa ni agizo la Wizara na Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda alifafanua walipewa agizo na wazo wamelifikisha kama lilivyo.

Hata hivyo, dakika chache baadaye Yanga nao wakatoa taarifa kwamba hawatambui kuahirishwa kwa mchezo huo ambao ulianza kuhudhuriwa na mashabiki tangu saa 3 asubuhi na kuujaza uwanja mapema tu.

Katika taarifa hiyo ya Yanga, ilisema ingepeleka timu uwanjani na kufuata taratibu na kama mechi haitaanza kama ilivyopangwa wangeondoka uwanjani kitu ambacho walikifanya, huku mashabiki wa klabu hiyo mapema wakiliamsha kwa kutoka uwanjani na kulalamikia ubabaishaji wa TFF na TPLB.

Yanga ilitinga uwanjani saa 10:15 jioni kisha mtunza vifaa kupanga saa 11:26 kabla ya robo saa baadaye wachezaji kutoka ili kupasha misuli, kabla ya kurudi tena vyumbani kubadilisha jezi na kuvaa zile za mechi na kurejea tena uwanjani saa 10:58 kupasha moto na ilipotimia saa 11:17 jioni timu iliaga baada ya mashabiki kuwakumbusha robo saa imeshatimia na kisha kuondoka zao.

Wakati wa kupasha wachezaji walikuwa wakipasiana wenyewe kwa wenyewe mpira kisha kufunga bao, kisha kwenda kushangilia kwenye kibendera na kuamsha shangwe uwanjani na walipotoka Yanga kwenda vyumbani Simba nao waliwasili uwanjani.

Mtunza vifaa wa Simba aliingia uwanjani saa 11:40 jioni kabla ya makocha wa timu hiyo wakiongozwa na Didier Gomes kuingia uwanjani dakika 10 baadaye na kutoka saa 11:54 jioni kabla ya nyota wa Simba kuingia kupasha saa 12:06 jioni wakiongozwa na kipa Aishi Manula na kuamsha shangwe kwa mashabiki wao.

Saa 12:15 jioni uwanjani kuliingia brass bendi ya jezi na kuamsha shangwe zaidi kwa mashabiki hao wa Simba walioujaza uwanja, lakini dakika mbili lilitolewa tangazo la kuahirishwa kwa mchezo hadi itakapotangazwa baadaye na kufanya mashabiki hao kupigwa na butwaa na kuanza kupiga kelele kutaka warudishiwe fedha zao za viingilio, huku wale wachache wa Yanga wakishangilia kwa furaha.

VIONGOZI WAKWEPA

Tukio la mechi ya Simba na Yanga kushindwa kufanyika kwa sababu zisizoeleweka ni kwa mara ya kwanza nchini na kufanya viongozi wenye dhamana ya mchezo huo kukwepa kutoa majibu ya kitu kilichokwamisha mpambano huo kufanyika huku ikiwa limewatia hasara watu wengine ikiwamo TFF.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuf Singo alipotafutwa na Mwanaspoti ili kutoa ufafanuzi juu ya taarifa kwamba wizara ndio iliyotaka mchezo kusogezwa mbele, alikataa kusema lolote kwa kudai kwamba alikuwa kikaoni.

“Tafadhali naomba uniache, nipo kikaoni kwa sasa, siwezi kujibu chochote,” alijibu kisha kukata simu, huku Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka (TFF), Salum Madadi akisema asingeweza kulizungumzia jambo hilo kwani lingetolewa tamko rasmi.

Hata hivyo, alipobanwa alisema TFF na Bodi watakuwa na kikao kesho Jumatatu ili kujadili na kulitolea tamko tukio hilo ambalo limeacha maswali mengi kwa wadau wa soka wakihoji kulikuwa na sababu gani TFF isitoe taarifa mapema kulingana na kanuni za ligi.

Viongozi wa juu wa Yanga hawakupatikana kwani waliondoka na timu uwanjani, huku Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez aligoma kuzungumza chochote juu ya kuahirishwa kwa mchezo huo kwa madai kwamba alikuwa na haraka.

MASHABIKI WAPIGWA MABOMU

Mara baada ya mechi hiyo kuahirishwa na mashabiki kuonekana kugoma kutoka uwanjani, taa zilizimwa na walipotoka nje waligoma kuondoka kwa kutaka warudishwe fedha zao kabla ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

mabomu pic

Mabomu hayo yaliwatawanya mashabiki hao waliokuwa wamejazana kwenye maeneo ya kuegesha magari na baada ya muda askari wakafanya doria kila kona kuangalia kama kuna wengine walikuwa wamesalia na wale waliokuwa kwenye magari yao walilazimishwa kujitambulisha na kuondoka haraka.

YANGA YAPEWA HEKO

Kitendo cha Yanga kuamua kuwahi mapema uwanjani, kisha kuondoka bila kusubiri muda mpya uliotangazwa kwa ajili ya mchezo huo, umepongezwa na baadhi ya wadau wakidai ni sahihi kwao kulingana na kanuni na sheria za soka.

Beki wa zamani wa kimataifa wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Bakari Malima alisema mtu aliyetoa amri ya kusogeza mechi mbele kutoka saa 11 jioni hadi 1:00 usiku anatakiwa kuwajibishwa kwani ni ishara ya kuwagawa Watanzania katika makundi mawili.

Malima alisema Yanga wamezingatia kanuni na sheria ya mchezo inavyotaka, hivyo kitendo cha TFF kuahirisha ikitoa sababu ya kupokea maelekezo ya wizara bila maelekezo yaliyoshiba sio tu cha kiungwana, lakini pia inaonyesha jinsi gani soka la Tanzania lina safari ndefu kufika mbali.

“Wanataka kumpa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu majaribu, angekuwa Hayati John Magufuli yupo hai angeishatoa tamko kabla ya Yanga kuondoka uwanjani,” alisema Malima.

“Aliyesababisha hayo anatakiwa achukuliwe hatua na aseme sababu ilikuwa ni nini hadi asogeze muda huo kiholela wakati anatambua upinzani mkali baina ya timu hizo.”

Naye beki mwingine wa zamani wa kimataifa wa Simba na Yanga, Godwin Aswile alisema kitendo kilichotokea ni aibu na hakina budi kuchukuliwa hatua kwa ajili ya afya ya soka la Tanzania, ili timu nyingine zisijisikie yatima.

“Kabla ya kutoa maoni TFF na wizara zitoe tamko, lakini pia hizi timu ziwe na viwanja vyao, hicho (cha Mkapa) ni cha serikali, kinachonisikitisha haki ya pesa za mashabiki zitapatikanaje, ambao wametoka mikoani kuja Dar es Salaam wanajisikiaje? Lazima ifikie hatua ya soka kuwa na nidhamu,” alisema Aswile.

Advertisement