Rekodi zazibeba Simba, Yanga

MACHO na masikio ya wadau wa soka nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yataelekezwa kwa Mkapa kunakopigwa mechi mbili za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ikianza keshokutwa Ijumaa dhidi ya Al Ahly, kisha Yanga na Mamelodi Sundowns kuvaana Jumamosi, huku rekodi tamu zikiwabeba wenyeji.

Presha ya michezo hiyo ni kubwa kwa mashabiki, wachezaji na hata mabenchi ya ufundi ya timu zote kutokana na ubora wa kila upande.

Miguel Gamondi kwa Yanga na Abdelhak Benchikha wa Simba wamebeba matumaini ya mamilioni ya Watanzania wanaoamini kama makocha hao watachanga vizuri karata zao, huenda ikaandikwa historia mpya katika soka la Tanzania na Afrika kwa jumla.

Licha ya mechi hizo zote kuonekana kuwa ngumu na kutotabirika kirahisi, lakini rekodi na takwimu zilizopo kwa timu zote nne katika michuano hiyo kuanzia raundi ya awali zinawabeba zaidi wenyeji.

Ipo hivi. Takwimu za Simba katika michezo mitano iliyopita ikiwa nyumbani zinaonyesha Mnyama ameshinda mechi tatu ambazo ni dhidi ya Jwaneng Galaxy F.C kwa mabao 6-0, Wydad Casablanca mara mbili 2-0 na 1-0, imetoa sare mbili dhidi ya Power Dynamos kwa bao 1-1 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa bao 1-1.

Katika michezo hiyo, Simba imefunga jumla ya mabao 11, ina wastani wa kupachika mabao mawili ikiwa nyumbani huku ikiruhusu mabao mawili.

Al Ahly katika michezo mitano iliyopita ugenini Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshinda mechi mbili, dhidi ya Medeama 1-0 na Kedus Giorgis 3-0, imetoa sare tatu, dhidi ya Belouizdad (0-0), Yanga (1-1) na Wydad Casablanca kwa bao 1-1.

Kwa kuangalia fomu ya timu zote mbili, Simba ikiwa nyumbani, Al Ahly ikiwa ugenini hakuna iliyopoteza, hivyo inaweza kuwa moja ya mechi ngumu na kwenye michezo ya mwisho kwa wababe hao kukutana zilitoka sare kwenye michezo yote miwili, wa kwanza ilikuwa sare ya mabao 2-2 kwa Mkapa na Mnyama, ilipokwenda Misri ilitoka sare ya bao 1-1 kwenye michuano mipya ya African Football League.

Yanga inaonekana kuwa ya moto zaidi ya Simba kwani katika michezo mitano ya nyumbani, imeshinda minne, dhidi ya Belouizdad 4-0, Medeama  3-0, Al Merreikh kwa bao 1-0 na dhidi ya ASAS kwa mabao 5-1, Wananchi wametoa sare moja tu ambayo ni dhidi ya Al Ahly.

Vijana wa Miguel Gamondi wamefunga jumla ya mabao 14, wana wastani wa kufunga wa 2.8, wameruhusu mabao mawili tu.

Mamelodi ikiwa ugenini katika michezo mitano iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshinda mechi tatu ambazo ni dhidi ya Nouadhibou kwa mabao 2-0, Pyramids 1-0, Bumamuru 4-0, wametoa suluhu moja na Wydad Casablanca na wamepoteza moja dhidi ya TP Mazembe 1-0.

Hata hivyo, pamoja na rekodi hizo tamu kwa Simba na Yanga, bado timu hizo zinapaswa kuwa makini na wapinzani wao, kwani zimekuwa zikibadilika kila hatua ya michuano hiyo na kwa Al Ahly kwa misimu mitano iliyopita ilipocheza robo fainali ni mara moja tu ilikwamia hapo.

Mechi nyingine nne ilifika hadi fainali na tatu kati ya hizo ilibeba taji na mara moja tu ilipoteza kuonyesha ni timu ya aina gani, huku ikiwa pia ndio watetezi wa taji kwa sasa.