Rekodi zambeba Nabi Derby

ANATOBOA hatoboi? Hilo ndilo linaloweza kuwa swali linalowachanganya mashabiki wa Yanga kwa sasa wakisaliwa saa chache tu kabla ya kumshuhudia Kocha Nasreddine Nabi akiwaongoza vijana wake kwenye mechi yake ya kwanza ya Kariakoo Dabi dhidi ya Simba.

Rekodi tamu za makocha waliomtangulia kwenye mapambano ya watani wa jadi, imewatia nguvu Wanayanga wakiamini Nabi naye huenda akatoboa, lakini wakiata ubaridi fulani wakiufikiria mziki wa Msimbazi unaoongoza msimamo wa Ligi Kuu, ikifunga pia mabao kibao.

Ni hivi. Kocha Nabi anaweza kuendeleza au kukutana na mwisho wa nyota ya bahati ambayo makocha wapya wa Yanga wamekuwa nayo katika miaka ya hivi karibuni dhidi ya Simba katika mchezo wa watani wa jadi utakaochezwa leo Jumamosi, kwenye Uwanja wa Mkapa.

Bahati hiyo ni ile ya Yanga kutopoteza mechi dhidi ya Simba huku wakiwa na kocha anayeiongoza kwa mara ya kwanza katika mechi inayozikutanisha timu hizo mbili kubwa nchini katika mashindano tofauti.

Ingawa Simba imekuwa ikipata ushindi dhidi ya Yanga mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, watetezi hao wa misimu mitatu mfululizo wameshindwa kuifunga Yanga pindi inapokuwa na kocha mpya akiwa analiongoza kwa mara ya kwanza benchi la ufundi la timu hiyo.

Upepo wa bahati kwa makocha wapya wa Yanga ulianzia kwa Mwinyi Zahera ambaye miezi minne baada ya kupewa kibarua cha kuinoa timu hiyo, aliishangaza Simba kwa kulazimisha nayo sare tasa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliochezwa Septemba 30, 2018. Licha ya kutopewa nafasi kubwa ya kupata hata sare katika mechi hiyo, Yanga ilionekana kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kuifanya Simba iliyokuwa na kikosi chenye washambuliaji walio na uchu wa kufumania nyavu itoke patupu.

Baada ya Yanga kuachana na Zahera, Novemba 8, 2019 ilimchukua nyota wake wa zamani, Boniface Mkwasa na kumpa jukumu la kuwa kocha wa muda wa kikosi ambacho Januari 4, 2020 kilikabiliwa na watani wa jadi wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu 2019/2020. Pamoja na Simba kutangulia kufunga mabao mawili katika mchezo huo ambao ulionekana wangeweza kuibuka na ushindi, Yanga iliwashangaza kwa kusawazisha kupitia kwa Mapinduzi Balama na Mohamed Hussein aliyejifunga na kufanya umalizike kwa sare ya mabao 2-2, huku yale ya Simba yakifungwa na Meddie Kagere na Deo Kanda. Mkwasa baada ya kuiongoza kwa muda Yanga, nafasi yake ilichukuliwa na kocha Mbelgiji, Luc Eymael ambaye kibarua chake cha kwanza dhidi ya Simba kilikuwa ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu uliochezwa Machi 8, 2020.

Katika mchezo huo, Simba ililala kwa bao 1-0 lililopachikwa na winga Bernard Morrison kwa mkwaju wa faulo uliotokana na faulo ambayo ilitolewa na refa Martin Saanya baada ya Jonas Mkude kumfanyia faulo nyota huyo wa Ghana.

Baada ya Eymael, Yanga ilimleta kocha Zlatko Krmpotic ambaye yeye hakupata fursa ya kukutana na Simba kwani aliiongoza timu hiyo katika mechi tano tu za Ligi Kuu na baada ya hapo akaonyeshwa mlango wa kutokea.

Kuondoka kwa Krmpotic kulifungua milango kwa Cedric Kaze ambaye kibarua chake cha kwanza dhidi ya Simba kilikuwa ni Novemba 7 ambapo aliiongoza timu yake kulazimisha sare ya bao 1-1, Yanga ikitangulia kupata bao la penalti ya Michael Sarpong, kisha Joash Onyango akasawazisha. Kwa rekodi hizo za makocha wa Yanga wanapovaana na Simba na kutofungwa inasubiriwa kuonwa kwa Nabi ambaye ndiye anaongoza jahazi la Jangwani.

Nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kukipiga Simba na Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisema mechi ya kesho ni ngumu kuitabiri, lakini akizungumzia juu ya matokeo ya Yanga dhidi ya Simba hasa pale turufu inpoonekana kuwang’aria Msimbazi na kibao kubadilika.

Mshambuliaji huyo na Mfungaji Bora wa muda wote katika Ligi Kuu Bara, alisema kujiamini kupitiliza ndiko kumekuwa kukiwaponza Simba tofauti na Yanga ambao huwa wanacheza kwa nidhamu na juhudi kubwa katika mechi hizo.

“Yanga huwa haipewi nafasi hivyo wachezaji wanajikuta na ile ari na morali ya kujituma ili kuthibitisha kuwa wao sio wanyonge ndio huwa inawafanya wapate matokeo mazuri lakini Simba huwa wanahisi watapata ushindi kirahisi hivyo inapelekea washindwe kupata kile wanachokitegemea,” alisema Mmachinga.