Rekodi za Ihefu Bara zashtua

Muktasari:

  • Ihefu FC ilisajili wachezaji saba dirisha dogo wakiwachukua Aboubakar Khomeiny, Kelvin Nashon, Manu Labota, Amade Momade, Marouf Tchakei, Joash Onyango na Elvis Rupia.

Licha ya kufanya usajili mkubwa dirisha dogo kikosi cha Ihefu FC bado kinasuasua kupata matokeo kwenye mechi saba walizocheza wamepata ushindi mechi moja tu, huku kocha Mecky Maxime akilia na ushindani.


Ihefu FC ilisajili wachezaji saba dirisha dogo wakiwachukua Aboubakar Khomeiny, Kelvin Nashon, Manu Labota, Amade Momade, Marouf Tchakei, Joash Onyango na Elvis Rupia.


Mastaa hao walichofanikiwa ni kuiondoa timu hiyo kwenye nafasi iliyokuwepo 15 na kuipandisha hadi nafasi ya 11 kenye msimamo ikiwa imekusanya pointi 24 kwenye mechi 22 walizocheza.


Katika mechi saba walizocheza chini ya kocha Mecky Maxime wameshinda mchezo mmoja, sare tatu na vipigo vitatu walianza Kagera Sugar ugenini wakipigwa mabao 2-1.


Mechi nyingine ni dhidi ya Mashujaa sare ya bao 1-1, walishinda bao 1-0 dhidi ya KMC, walikubali kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Yanga, wakapoteza dhidi ya Coastal Union bao 1-0, sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba na 1-1 dhidi ya Ihefu FC.


Akizungumza na Mwanaspoti, Maxime alisema ni kweli timu inapambania matokeo licha ya kujaa mastaa wengi kikosini huku akikili kuwa ni sehemu ya matokeo.


"Dirisha dogo ni kweli kulikuwa na maingizo mengi na timu imeanza na mimi nikiwa kocha mpya kikosini hivyo mikakati ni kuona timu inakuwa na kikosi imara na cha ushindani hilo haliwezi kuanza moja kwa moja lazima kuwena changamoto hilo kama benchi la ufundi tumeliona," alisema na kuongeza;


'Ubora wa wachezaji ni mkubwa na kila mchezaji anahali ya kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo sasa tunachokiangalia zaidi ni kuibakiza timu ligi kuu msimu ujao mambo mengine yatafuata." Alisema.


Maxime alisema timu kidogo kidogo inapata muunganiko na maelewano mazuri anaamini matokeo wanayoyapata yanachangiwa na ugumu wa mzunguko wa pili huku akikiri kuwa bado anaimani na kikosi chake.

MECHI ZILILOBAKI
Azam FC vs Ihefu FC
Ihefu FC vs Namungo
Ihefu FC vs JKT Tanzania
Tanzania Prisons vs Ihefu FC
Tabora United vs Ihefu FC
Ihefu FC vs Dodoma Jiji
Ihefu FC vs Mtibwa Sugar