Rekodi yaibeba Namungo kwa CD de Agosto

Dar es Salaam. Ushindi wa kwanza waliopata Namungo wa kuifunga CD de Agosto mabao 6-2, ni kama vile tayari timu hiyo imeanza kujiweka katika nafasi nzuri kwenye hatua ya mtoano wa kombe la Shirikisho Afrika.

Licha ya kwamba mchezo huo ulichezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Namungo ilikuwa ugenini hiyo ni baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuamua mechi zote mbili kuchezwa Tanzania baada ya matatizo ya mamlaka za Angola juu ya ugonjwa wa COVID-19.

Namungo iliibuka na ushindi kutokana na hali ya kujihisi ipo nyumbani.

Wakiwa nyumbani katika Kombe la Shirikisho, Namungo hawajawahi kupoteza, hasa wanapokuwa Uwanja wa Azam Complex.

Namungo ikiwa nyumbani imecheza mechi mbili za Kombe la Shirikisho na kushinda zote.

Ilicheza dhidi ya Al Rabita kwenye raundi ya awali walishinda 3-0 kisha dhidi ya Hilal Obayed katika raundi ya kwanza na walishinda 2-0 mechi zote zikichezwa katika Uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya De Agosto utakaopigwa leo, Namungo itakuwa nyumbani huku ikiwa na mtaji wa mabao sita iliyopata ugenini.

Rekodi na mabao hayo yanaibeba Namungo ikiwa nyumbani, lakini pia fursa ya mashabiki kuingia itakuwa chachu zaidi ya ushindi kwao.

Kocha wa Namungo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema bado wana kazi ya kufanya katika mchezo huu wa marudiano kuhakikisha wapinzani wake hawapati magoli kama ilivyokuwa mchezo wao wa kwanza.

“Tulifanya makosa kadhaa na hapo hapo wenzetu walitufunga kwenye mechi hii nitahakikisha tunafuta makosa ambayo tumeyafanya kwenye mchezo uliopita.

Morocco pia alisema katika mchezo uliopita walitengeneza nafasi nyingi lakini walizitumia chache.

Kama Namungo itafanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho itakuwa imejihakikishia kupata fedha kwani kuingia makundi hata ukimaliza nafasi ya nne bado unapata fedha.

Ukimaliza nafasi ya nne katika makundi unapata zawadi ya Dola za kimarekani 275,000 ambazo ni sawa na Sh637,725,005, huku kama akimaliza nafasi ya tatu basi atapata fedha hizo hizo.